Rais wa Korea Kusini Yoon anusurika kung'olewa madarakani
7 Desemba 2024Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol amenusurika kung'olewa madarakani katika hoja iliyowasilishwa bungeni na upinzani nchini humo baada ya amri aliyotangaza ya sheria ya kijeshi mapema wiki hii. Rais Yoon amenusurika baada ya wanachama wa chama chake kususia kura hiyo.
Spika wa bunge la nchi hiyo ametangaza kwamba idadi ya kura zilizopigwa hazikutosha kuifanya kura hiyo kuhesabiwa. Kura 195 pekee ndizo zilizopigwa na kura 200 zilihitajika ili kuhesabika kwa kura hiyo.
Soma zaidi: Rais Yoon wa Korea Kusini aomba radhi kwa raia wake
Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Party kimesema kitaifufua tena hoja hiyo ya kumfungulia mashtaka hapo wiki ijayo hata kama imeshindikana hii leo.
Hata hivyo, Rais Yoon Suk Yeol alilihutubia taifa hilo asubuhi ya leo na kuomba radhi kwa taifa lake kutokana na amri aliyotangaza ya sheria ya kijeshi mapema wiki hii, hatua ambayo ilizua ukosoaji mkubwa dhidi yake.