Ripoti ya WHO kuhusu Malaria
18 Septemba 2008Shirila la afya ulimwenguni WHO leo limetoa ripoti yake ya mwaka kuhusu ugonjwa wa malaria duniani.Ripoti hiyo inasema kwamba inakadiriwa watu millioni 247 waliambukizwa ugonjwa huo katika mwaka 2006. Idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na makadirio yaliyotolewa awali. hata hivyo mkuu wa WHO Margaret Chan amesema ukusanyaji wa data juu ya ugonjwa huo bado unafanyika katika kiwango kibaya katika nchi nyingi.
Ripoti hiyo ya shirika la afya ulimwenguni inasema kuwa jumlya ya nchi 109 zimeaathiriwa na ugonjwa wa malaria katika mwaka 2008 na kiasi nusu ya nchi hizo ni za afrika.Nchi nyingi zinakosa uwezo wa kutosha wa kukabiliana na ugonjwa.Pamoja na kwamba vituo vya huduma za matibabu ya umma vinapokea dawa za kukabiliana na Malaria,bado matibabu hayo hayatoshi katika nchi zote.
Ripoti ya mwaka kuhusu ugonjwa wa malaria duniani imesema kwamba katika nchi zote ambako kulifanyika uchunguzi juu ya maradhi hayo imebainika kwamba watu wengi hawapati matibabu ya ugonjwa huo ingawa kuna hatua zilizopigwa katika kupamabana na Malaria.
Ripoti hiyo pia inasema watu millioni 247 waliambukizwa ugonjwa wa malaria katika mwaka 2006 duniani kote idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na makadirio yaliyotolewa mwanzo na serikali na makampuni ya kutengeneza dawa ambapo ilikadiriwa watu millioni 350 hadi millioni 500 wanaambukizwa kila mwaka ugonjwa wa Malaria.
Ripoti hiyo mpya pia imepunguza idadi ya vifo vinvyotokana na ugonjwa huo duniani ikilinganishwa na matokeo ya shirika hilo yaliyotolewa katika ripoti yake ya miaka mitatu iliyopita ambapo idadi hiyo ya vifo imeonekana kupungua kwa asilimia 10.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ni kwamba watu 881,000 wamekufa kutokana na ugonjwa wa malaria katika mwaka 2006 ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo ilikadiriwa zaidi ya watu millioni 1 hufa kila mwaka kutokana na malaria wengi ikiwa ni watoto wachanga na kina mama wajawazito.
Kiasi kikubwa cha fedha kimekuwa kikitolewa katika miaka iliyopita kupitia shirika la WHO,pamoja na mashirika mengine makubwa kukabiliana na ugonjwa wa malaria.Kutokana na hali hiyo mkuu wa shirika hilo la WHO Margaret Chan amefahamisha kwamba ripoti kuhusu malaria itakuwa inatolewa kila mwaka ili wanaopitisha maamuzi waweze kupata maelezo sahihi kuhusiana na ugonjwa huo.
Aidha Chan ametoa mwito kwa makampuni ya kutengeneza madawa kuongeza juhudi katika utafiti wa kutafuta dawa ya Malaria kutokana na ripoti zinazotolewa kwamba baadhi ya wagonjwa wameanza kuonyesha dalili za mwili kuwa sugu, ikiwa na maana dawa hizo kushindwa kufanya kazi.
Ugonjwa wa malaria unawaathiri watu wengi barani Afrika.Ripoti ya shirika la afya ulimwenguni WHO inasema kuwa nchi za Nigeria,Jamhuri ya kidemokrasi ya kongo, Uganda , Ethiopia na Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokuwa na idadi kubwa ya vifo vilivyosababishwa na ugonjwa wa malaria katika mwaka 2006.
Mbali na Afrika mataifa mengine yaliyotajwa kuathiriwa zaidi na ugonjwa huo mwaka 2006 ni pamoja na India,Bangladesh na Indonesia.