Russia yaigusa pabaya Ukraine, Kyiv yajibu mapigo
20 Desemba 2024Jeshi la anga la Ukraine limesema lilizuwia makombora matano ya Iskander yaliyolenga mji huo, lakini mashambulizi yaliharibu huduma za upashaji joto katika majengo 630 ya makazi, vituo 16 vya matibabu, na shule na vituo vya kulelea watoto 30, huku mabaki ya makombora hayo yakisababisha moto na uharibifu katika wilaya tatu.
Mabaki ya makombora yaliyodondoka Kyiv yaliharibu majengo ya ofisi kadhaa, Kanisa Katoliki la Mt. Nicholas ambalo ni alama ya mji huo, na Chuo Kikuu cha Lugha cha Kyiv.
Mawimbi ya mlipuko pia yalivunja madirisha au kusababisha uharibifu kwenye balozi sita, kulingana na Heorhii Tykhyi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine.
Soma pia: Wakuu wa Umoja wa Ulaya wajadiliana vita vya Ukraine na suala la Syria
"Leo mjini Kyiv, shambulio la kombora liliharibu balozi kadhaa zikiwemo za Albania, Argentina, Palestina, Macedonia Kaskazini, Ureno, na Montenegro, zote zikiwa kwenye jengo moja lililoharibiwa vibaya," alisema Tykhyi huku akionesha za magari na ofisi zilizoharibiwa.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amelaani shambulio hilo, akisema ni mfano mwingine wa dharau ya Rais Vladmir Putin kwa sheria za kimataifa.
Shambulizi la kisasi kwa matumizi ya silaha za magharibi
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema shambulio lake lilikuwa kisasi kwa shambulio la Ukraine katika mkoa wa Rostov, ambako ilitumia makombora sita ya ATACMS kutoka Marekani na manne ya Storm Shadow kutoka Uingereza.
Ukraine ilisema shambulio hilo lililenga kiwanda cha mafuta cha Rostov kama sehemu ya kampeni yake ya kushambulia miundombinu ya Urusi inayosaidia juhudi za vita.
Soma pia: Urusi yadai kumzuilia mshukiwa aliyemuua Igor Kirillov
Ukraine ilianza kutumia makombora ya masafa marefu iliyopewa na Marekani mnamo Novemba 19, baada ya Washington kulegeza vikwazo vya matumizi yake.
Hatua hiyo ilisababisha Urusi kutumia kombora jipya la Oreshnik, ambalo Putin alisema linaweza kulenga majengo ya serikali Kyiv, ingawa halijaripotiwa kutumika tena.
Katika kujibu, Urusi ilifanya shambulio kubwa kwa kutumia silaha za kisasa za masafa marefu dhidi ya kituo cha ujasusi cha kijeshi cha Ukraine na mifumo ya makombora ya Neptune, huku pia ikilenga mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot kutoka Marekani.
Urusi ilidai kufanikisha shabaha zote, madai ambayo hayajathibitishwa.
Kombora la Ukraine laua sita mkoa wa Kursk
Watu sita, wakiwemo mtoto mmoja, wameuawa Ijumaa katika shambulio la kombora la Ukraine kwenye mji wa Rylsk, mkoa wa Kursk, Urusi, kwa mujibu wa kaimu gavana Alexander Khinshtein.
Majeruhi 10, wakiwemo mtoto wa miaka 13, wamepelekwa hospitalini kwa majeraha madogo.
Khinshtein aliilaumu Ukraine kwa kushambulia raia kwa makusudi, akisema waliohusika watapata "adhabu wanayostahili."
Soma pia: Trump aahidi tena kumaliza "mauaji" ya vita vya Ukraine
Shambulio hilo liliharibu shule, kituo cha burudani, na nyumba binafsi. Urusi imesema itajadili suala hili katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Tangu Agosti 6, wanajeshi wa Ukraine wanadhibiti sehemu ya mkoa wa Kursk baada ya kuvuka mpaka kwa mshangao.
Rais Putin amesema wanajeshi hao wataondolewa, lakini hakutoa tarehe ya lini hilo litatokea.
Tuhuma za kushambulia raia zimeongezeka kati ya pande zote mbili zinazopinga madai hayo.
Kyiv yapokea miili ya wanajeshi 503 waliouawa vitani
Ukraine imesema Ijumaa kuwa imepokea miili ya wanajeshi 503 waliouawa kutoka Urusi, ikiwa ni sehemu ya urejeshaji wa nadra wa miili ya wanajeshi kati ya Moscow na Kyiv tangu vita kuanza mwaka 2022.
Kati ya miili hiyo, 403 ilitoka eneo la Donetsk, huku mingine ikitoka Lugansk, Zaporizhzhia, na majokofu ya Urusi.
Soma pia: Urusi yashambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine
Urejeshaji huu, wa nne tangu Oktoba, unaonyesha gharama kubwa ya vita ambavyo vimeendelea kwa karibu miaka mitatu.
Rais Zelensky alisema mwezi huu kuwa wanajeshi 43,000 wa Ukraine wameuawa na 370,000 wamejeruhiwa tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza.
Urusi haijatoa taarifa kuhusu idadi ya wanajeshi wake waliouawa wala urejeshaji wa miili yao.
Chanzo: Mashirika