1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la kigaidi la Manchester lagonga vichwa vya habari

Oumilkheir Hamidou
24 Mei 2017

Shambulio la kigaidi la Manchester, ziara ya rais wa Marekani Donald Trump Mashariki ya kati na mzigo wa madeni ya Ugiriki ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazetini ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/2dV0r
UK | Trauerbekundungen nach dem Anschlag in Manchester
Picha: picture-alliance/empics/D. Lawson

Tunaanzia Uingereza ambako shambulio la jumatatu katika tamasha ya muziki ya  muimbaji Ariana Grande, mjini Manchester linaendelea kugonga vichwa vya habari. Wahariri wanakubaliana shambulio hilo linazidi kupanua ufa ulioko kati ya wale wanaounga mkono na wale wanaopinga mchanganyiko wa jamii tofauti nchini Uingereza. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika: " Madhara makubwa yanasababishwa na mashambulio ya Manchester na sio tu kwa wahanga na familia za wahanga. Ikiwa mashambulio dhidi ya kituo cha usafiri wa chini kwa chini , miaka 12 iliyopita mjini London yalisababisha nchi hiyo ya kifalme kuwa kitu kimoja, inahofiwa haya ya Manchester yatapelekea ufa ulioko katika jamii uzidi kuwa mpana. Shambulio la Manchester litashawishi kampeni za uchaguzi unaokuja wa baada ya Brexit, na hitilafu zilizoko nchini humo zitazidi kuwa kubwa. Tokea hapo waingereza wa maeneo ya mashambani ambao ni wahafidhina wanashindwa kukubaliana na wenzao wa mijini ambao ni waliberali kama uhamiaji na ukarimu ni jambo baya au la baraka. Ni jambo la kutegemea kuona yaliyotokea Manchester yakimpatia nguvu Theresa May na sera zake za kujitenga. Mashambulio ya kigaidi ya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam yanaonyesha kulifikia lengo lake, nalo ni kuubadilisha mtazamo wa nchi za magharibi."

Matumaini ya amani Mashariki ya kati

Ziara ya rais wa Marekani Mashariki ya kati nayo pia imemulikwa magazetini. Gazeti la "Mitteldeutsche" la mjini Halle linaandika: "Hata kama ila rais Trump anazoitia Iran zinatia hofu, hata hivyo kwa Israel hakuna wakati muwafak zaidi ya huu kuanzisha duru mpya ya mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati. Ni jukumu la Netanyahu kuitumia fursa iliyojitokeza. Anategemewa yeye tu kama mkutano wa amani uitishwe au la. Cha kuwekewa suala la kuuliza pia ni kama Donald Trump ni wa kutegemewa au la."

Mdaiwa na wanaodai wakubaliane kuhusu mzigo wa madeni ya Ugiriki

 Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mzigo wa madeni ya Ugiriki. Gazeti la Donaukurier linaandika: "Wahariri wanakubaliana shinikizo linabidi liendelezwe kuitaka Ugiriki iendeleze mageuzi. Hata hivyo wanasema wadau wa kanda ya Euro pia wanabidi watambue bila ya kutoa ridhaa,kamwe Athens haitoweza kuupunguza mzigo wa madeni yanayofikia Euro bilioni 314."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman