Shambulizi Yemen lawaua watu 35
23 Agosti 2017Zaidi ya watu 30 wameripotiwa kuuawa miongoni mwao raia kufuatia mashambulizi ya kutoka angani Kaskazini ya mji mkuu wa Yemen, Sanaa. Juhudi za uokozi zinaendelea katika majengo ambayo yilishambuliwa. Waasi wa kundi la Huthi wanaoungwa mkono na Iran, wamedai muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ndio umefanya mashambulizi hayo. Mkuu wa shirika la Hilal Nyekundu tawi la Sanaa Hussein al-Tawil amesema kuwa kuna miili ambayo imefunikwa kwenye vifusi.
Shambulio moja lililenga hoteli ambayo ilikaliwa na wafanyakazi wa shamba la miraa lililoko karibu. Hayo ni kwa mujibu wa meneja wa hoteli hiyo Taher al-Ahdal. Wakaazi wamesema waasi wa kundi la Huthi pia wamekuwa wakiishi katika eneo hilo. Hakuna mtu au kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo ambalo pia limewajeruhi watu 13.
Juhudi za uokozi
Ali Alrakmi ambaye ni daktari msaidizi anayeshiriki juhudi za uokozi amesema "Jengo lililolengwa ni hoteli ndogo inayowahifadhi wakulima 100 wanaovuna miraa. Tumepata miili 35, mingi yao imekatika vipande vipande, na bado kuna miili zaidi imefunikwa kwenye vifusi.”
Wahuthi ambao wanaudhibiti mji wa Sanaa kwa ushirikiano na wanajeshi wa Rais Ali Abdullah Saleh wameulaumu muungano wa kijeshi wa Kiarabu unaounga mkono serikali kuwa ndio umefanya shambulizi hilo katika wilaya ya Arhab.
Dai la waasi kuwa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umefanya shambulizi hilo limetangazwa kwenye runinga yao ya Al-Massira. Msemaji wa muungano huo hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.
Makundi ya kutetea haki za kibinadamu yameushutumu muungano huo mara kadhaa kufuatia mauaji ya raia kutokana na mashambulizi yao katika operesheni zao kuisaidia serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa tangu Machi 2015.
Takwimu za Umoja wa Mataifa
Tangu wakati huo, takwimu za Umoja wa Mataifa, zinasema kuwa zaidi ya raia 10,000 wamefariki na milioni tatu wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Tawif Ziad ni mkaazi wa Sanaa na analaani shambulizi la hivi karibuni. "Kuna binamu zangu 4 au 5 ambao bado wamefunikwa kwenye vifusi. Sote tunatoka mji mmoja. Hili shambulizi si kitendo ambacho Muislamu anapaswa kufanya”
Mashirika ya Amnesty International na Human Rights Watch yamezitaka Marekani, Uingereza na Ufaransa kukoma kuipa Saudi Arabia mabomu yao na silaha nyinginezo kufuatia kuuawa kwa raia.
Wakati huohuo, mizozano kati ya miungano ya Wahuthi na Saleh imeibua hofu ya kuzuka kwa makabiliano ya makundi hayo. Saleh anadai kuwa waasi wamemtenga na wapambe wake na kuwaacha nje katika maamuzi ya kijeshi na kisiasa pamoja na mazungumzo yanayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa ili kumaliza vita hivyo.
Mwandishi: John Juma/ AFPE/APE
Mhariri:Josephat Charo