1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sherehe za Mwaka Mpya zaingia dosari kufuatia Gharika ya Tsunami.

Charles Hilary31 Desemba 2004

Sherehe za mwaka mpya wa 2005 ambapo hivi sasa nchi nyingi zinalalia dago kuukaribisha safari hii zimeingia dosari kwa baadhi ya mataifa kutokana na kuwafikiria waathirika wa gharika iliyopiga Barani Asia.Mataifa mengi yamefuta katika ratiba zao shamra shamra na Australia inatarajiwa kuiongoza dunia katika dakika moja ya kukaa kimya kuwakumbuka waliokufa Asia.

https://p.dw.com/p/CEHC
Waathirika wa tsunami nchini India baada ya kupatiwa msaada wa chakula.
Waathirika wa tsunami nchini India baada ya kupatiwa msaada wa chakula.Picha: AP

Mji wa Sydney nchini Australia ambao ni mji mkuu wa awali duniani kusherehekea kuingia mwaka mpya wa 2005,umeamua kuendelea na sherehe hizo na hivi sasa wameshavurumisha fashfash muda si mrefu uliopita,lakini hata hivyo watu waliojazana kando ya bandari kuangalia anga ikihinikizwa fahsfash hizo wametakiwa kuwakumbuka watu wanaofikia 124,000 waliopoteza maisha yao barani Asia.

Mkasa wa gharika ya tsunami barani Asia umegubika kwa kiasi kikubwa shamrashamra za kuukaribishwa mwaka mpya hasa kwa mataifa ya Ulaya .Raia wa mataifa ya Ulaya ambao walikuwa ni watalii wanaongoza kwa idadi ya wageni waliokufa kutokana na mkasa huo.Ni zaidi ya watalii 2,200 kutoka Ulaya wamekufa kufuatia kadhia hiyo na wengine 6,000 bado hawajulikani walipo.

Sweden,Norway,Finland na Ujerumani zitapeperesha bendera za nchi zao nusu mlingoti usiku wa kuuanza mwaka mpya ikiwa ni ishara ya kutoa heshima kwa raia wao waliopoteza maisha katika gharika ya tsunami ambao waliiacha baridi kali ikiambatana na theluji nzito kwenda kulisaka jua na mchanga wa dhahabu katika fukwe za bahari za Asia.

Halikadhalika raia wa Australia watakaokwenda katika sherehe za kuualika mwaka mpya wameombwa kufikiria kuwachangia waathirika wa tsunami kupitia mfuko wa Oxfam.Kwa mujibu wa Meya wa mji wa Sydney katika mkesha wa mwaka mpya wanatarajia kukusanya dola milioni 3.9.Amesema huu ni wakati wa kuonesha urafiki wa kweli na kuwasaidia majirani zao wa Asia walio katika majonzi makubwa.

Katika sehemu nyingine duniani sherehe za mwaka mpya zimefutwa kabisa.Mfano nchini Sri Lanka ambapo hadi sasa watu 28,500 wamekufa kutokana na gharika ya tsunami, hoteli ya kifahari ya Hilton Colombo imefuta dansa lililokuwa lisakatwe katika mkesha wa mwaka mpya.Huko Thailand nchi hiyo imekataza kufanyika sherehe za mwaka mpya katika kuwakumbuka watu wanaofikia 4,500 waliokufa il hali Malaysia nayo haitakuwa na sherehe rasmi za mwaka mpya.

Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong ameamrisha kufutwa kwa sherehe za urushaji fataki katika ghuba ya Marina.Nako Hong Kong ambapo kwa kawaida sherehe za mwaka mpya huhusisha maandamano ya kuipinga serikali,vyama vya siasa katika kisiwa hicho vimeamua kuahirisha maandamano kama hayo na badala yake watafanya harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya waathirika wa tsunami.

Katika nchi za Ulaya hasa miji ya Italia nako sherehe za mwaka mpya zimesimamishwa na kitakachofanyika ni kwa fedha ambazo watu waliziandaa kwa sherehe hizo kuzichangia katika mfuko wa kusaidia watu wa bara la Asia waliofikwa na madhila ya tsunami.

Hapa nchini Ujerumani karibu na lango la Brandenburg Berlin mahali ambapo watu wanaofikia milioni moja hukusanyika kwa ajili ya sherehe za mwaka mpya,bendera zimekuwa zikipeperuka nusu mlingoti huku Wajerumani bado wakiwa katika majonzi makubwa kufuatia mkasa wa tsunami.

Raia wa Norway wametakiwa kuukaribisha mwaka mpya kwa kiasi na vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeripoti kuwa tajiri mkubwa nchini humo bilionea Kjell Inge Rokke amefuta maonesho yake ya kurusha fataki.

Nako katika kisiwa cha bahari ya Mediterranean cha Cyprus sherehe za mwaka mpya zimefutwa na fedha ambazo watu wa huko walipanga kuzitumia kwa ajili ya kuukaribisha mwaka mpya katika mji wa Nicosia pia mji wa bandari wa Limassol zitakwenda katika mfuko wa kuwasaidia waathirika wa gharika ya tsunami.

Hakika dunia nzima imekumbwa na majonzi makubwa na kuguswa na gharika ya tsunami.Mungu atujalie mwaka wa 2005 uwe wa baraka na amani.