1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier rais mpya wa Ujerumani

12 Februari 2017

Waziri wa zamani wa mambo ya nje Frank -Walter Steinmeier amechaguliwa kuwa rais mpya wa Ujerumani Jumapili (12.02.2017) wadhifa wa heshima ambao hauna madaraka makubwa ya utendaji.

https://p.dw.com/p/2XQi3
Bundespräsidendentenwahl Merkel gratuliert Frank-Walter Steinmeier
Picha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 61 ambaye mara kwa mara uchunguzi wa maoni umekuwa ukimuonyesha kuwa ndie mwanasiasa mashuhuri kabisa nchini ataliwakilisha taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya nchi za nje na atatumika kama mtu mwenye kuheshimika na kuaminika kwa taifa.

Wanachama wenzake wa chama cha Social Demokrat (SPD) wanataraji kuchaguliwa kwake kutaimarisha nafasi yao wakati mgombea wao Martin Schulz spika wa zamani wa bunge la Ulaya akijitayarisha kupambana na Kansela Angela Merkel kuwania ukansela katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi wa Septemba.

Apata kura 931

Reichstag in Berlin Bundesüräsident Steinmeier Antrittsrede
Frank-Walter Steinmeier akihutubia bungeni.Picha: Reuters/F. Bensch

Steinmeier amepata kura 931 kati ya 1,260 zilizopigwa baada ya mmugano wa kihafhidhina wa Merkel kukosa mgombea wao wenyewe aliye imara kukubali kumuunga mkono kuchukuwa nafasi ya Joachim Gauck mchungaji wa zamani mwenye umri wa miaka 77 kutoka iliokuwa Ujerumani mashariki.

Kura hiyo imepigwa katika bunge la Ujerumani mjini Berlin katika kikao maalum cha bunge la shirikisho kilichowajumuisha wabunge wa taifa na wawakilishi kutoka majimbo 16 ya Ujerumani wakiwemo wabunge na pia wasanii,waandishi, wanamuziki na kocha wa timu ya soka ya taifa Joachim Loew.

Steinmeier mmojawapo wa wanasiasa mashuhuri nchini Ujerumani ametumika mara mbili kama waziri wa mambo ya nje chini ya utawala wa Merkel kwa jumla ikiwa ni miaka saba.

Juu ya kwamba mwanasheria huyo ni mtu muangalifu  wakati akitowa hotuba zake wakati wa kampeni ya mwaka jana ya  urais wa Marekani alimwita Donald Trump kuwa "mhubiri wa chuki"

Baada ya tajiri huyo kushinda uchaguzi Sreinmeier amesema uhusiano utakuwa mgumu na kwamba wafanyakazi wake walikuwa wakihangaika kupata ufasaha wa msimamo wa Trump katika sera yake ya kigeni.Steinmeier atashika wadhifa huo Machi 19.

Gauck apongezwa

Deutschland | Wahl des Bundespräsidenten | Joachim Gauck
Rais anayeondoka madarakani Joachim Gauck akishangiliwa.Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Spika wa bunge la Ujerumani Norbert Lamert amewakaribisha wabunge 1,260 bungeni mjini Berlin kwa ajili ya kumchaguwa mtu wa kushika nafasi ya Rais Joachim Goacja ambaye amejiuzulu kutokana na umri wake kuwa mkubwa. Mwanzoni mwa kikao hicho cha bunge cha 16 kwa mara nyengine tena spika huyo amempongeza rais huyo anayeondoka madarakani katika hotuba ya kusisimuwa ambapo amesema "Mshikamano wa raia ulikuwa muhimu sana kwake" Gauck pia amekuwa akisisitiza mara kwa mara jamii haipaswi kuhofu au kugawika hata wakati huu wa vitisho vya magaidi.Gauck alieonekana kuguswa na wabunge na wawawakilishi wengine wa majimbo waliokuwa wakimshangalia ukumbini.

Frank - Walter Steinmeir wa chama cha Social Demokratic anataka kupambana na kuongezeka kwa hali ya wasi wasi katika jamii wakati atakaposhika wadhifa huo  wa juu wa taifa.Akizungumza katika mapokezi ya chama chake katika bunge hilo la shirikisho  amesema "Ningelipenda kusema kwamba changamoto ni kubwa kwamba hatuwezi kuendelea nayo migogoro na mizozo inayotuzunguka."

 

 

Kuchaguliwa kwake kulikuwa na uhakika 

Deutschland | Wahl des Bundespräsidenten | Frank-Walter Steinmeier
Frank -Walter Steinmeier akipiga kura yake.Picha: picture-alliance/dpa/G. Fischer

Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel amevishukuru vyama vyengine waliounga mkono ugombea wa Steinmeier katika wadhifa huo jambo ambalo halijitokezi katika mwaka wa uchaguzi.Katika mkutano maalum wa chama cha SPD wa bunge ametangaza uteuzi huo wa Steinmeier kwa wadhifa huo ni zawadi ya kumuaga ya chama chake.

Tokea mwanzo kuchaguliwa kwa Steinmeier kwenye wadhifa huo kulikuwa ni jambo la uhakika:  waziri huyo wa mambo ya nje wa zamani alikuwa akiungwa mkono na mmungano wa kihafidhina wa vyama ndugu vya CDU na CSU ambavyo vina wingi wa viti bungeni.

Chama cha sera kali za mrengo wa kushoto  Die Linke,chama cha sera kali za mrengo wa kulia Chama Mbadala kwa Ujerumani AfD na kile cha Pirate vilikuwa na wagombea wao lakini havikuwa na nafasi kabisa ya  kushinda.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ dpa/AFP/ Reuters/DW

Mhariri : Lilian Mtono