1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yauonya Umoja wa Ulaya kuhusu wahamiaji

25 Februari 2016

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ametishia kuyakwamisha maamuzi katika mkutano ujao wa kilele wa Umoja wa Ulaya kama nchi wanachama hazitakubali kuchukua wahamiaji. Kauli yake imekuja baada ya mkutano wa Vienna.

https://p.dw.com/p/1I1Sb
Griechenland Parlament Premierminister Alexis Tsipras
Picha: picture-alliance/dpa/O. Panagiotou

Akizungumza bungeni jana (24.02.2016) Tsipras alisema haikubaliki kwa washirika wa Umoja wa Ulaya kuiachia Ugiriki mzigo mkubwa wa wakimbizi kuliko uwezo wake. Amesema hawatakubali baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya kujenga uzio na kuta bila kukubali hata mhamiaji mmoja. Waziri mkuu huyo pia amesema Ugiriki itataka nchi za Umoja wa Ulaya zilazimishwe kushiriki katika mpango wa kugawana wakimbizi.

Tsipras amesema Ugiriki haitoridhia makubaliano mpaka nchi za Umoja wa Ulaya zishiriki kisawasawa katika kuwahamisha na kuwapa makazi wakimbizi wanaowasili barani Ulaya. "Kile ambacho hatutakifanya ni kukubali nchi yetu kugeuka kuwa ghala la kudumu kwa binaadamu, huku wakati huo huo tukiendelea na shughuli barani Ulaya na katika mikutano ya kilele kana kwamba hakuna chochote kinachoendelea."

Kiongozi huyo amesema makubaliano yaliyopo ya umoja huo kuhusu kuwachukua wakimbizi sharti yatekelezwe bila kuchelewa, na ameikosoa Austria kwa kuwazuia wakimbizi.

Westbalkan Konferenz Sebastian Kurz Johanna Mikl-Leitner Wien Österreich
Waziri wa mambo ya ndani wa Austria, Johanna Mikl-Leitner (kushoto) na waziri wa mambo ya nje Sebastian Kurz (kulia)Picha: Getty Images/AFP/H.Fohringer

Tsipras ameyasema hayo baada ya mkutano wa mataifa ya Balkan uliondaliwa jana na Austria mjini Vienna. Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu "Kuudhibiti Uhamiaji kwa Pamoja" uliandaliwa kwa muda mfupi, ikiwa ni ujumbe kwa Ugiriki na Umoja wa Ulaya. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Austria, Sebastian Kurz, alisema Ugiriki ilikataa kuilinda mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya na inaendelea kuwaruhusu wakimbizi kusafiri Ulaya. Waziri huyo aidha alisema kwa kuwa Umoja wa Ulaya bado hauna suluhisho la pamoja kwa tatizo hilo, Austria haina chaguo lengine bali kuishughulikia hali hiyo katika ngazi ya kitaifa.

Mawaziri wa mambo ya nchi za kigeni kutoka Albania, Bosnia-Herzegovina, Bulgaria, Kosovo, Macedonia, Montenegro, Serbia na Slovenia walialikwa kuhudhuria mkutano huo wa siku moja.

Ujerumani lazima ichague

Tunataka kupunguza wimbi la wakimbizi. Mpaka sasa wakimbizi wameletwa Ulaya ya Kati. Sasa hatuwezi kukabiliana na idadi. Tumeweka kikomocha wakimbizi 37,500 mwaka huu; idadi hiyo badi ni kubwa ikilingansiwha na mataifa mengine ya Ulaya," akasema Kurz.

"Ujerumani inalazimika kuamua ni ishara gani inazotaka kuzitoa. Bado wanaonyesha ishara ya kuruhusu sera ya mipaka wazi kwa Ugiriki, lakini wanatarajia Austria izuie wimbi la wakimbizi. Hizi ni ishara mbili tofauti," alisema waziri wa mambo ya ndani wa Austria, Johanna Mikl-Leitner. "Lazima kuchagua mkakati mmoja na nafikiri mkutano huu umeonesha tunafanyia kazi lengo moja; kupunguza wimbi la wakimbizi."

Mkutano wa Vienna bila Ugiriki

Ugiriki haikualikwa, hatua iliyosababisha ghadhabu na ukosoaji kutoka viongozi wa nchi hiyo. Wanasiasa wanahofia maamuzi yatakayozidi kuifanya hali ya wasiwasi katika mpaka kati ya Ugiriki na Maceonia kuwa mbaya.

Siku ya Jumanne wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ugiriki ilitangaza imewasilisha malamiko ya kidiplomasia kupinga mkutano uliondaliwa na Austria. Wizara hiyo ilisisitiza mkutano huo kuhusu wakimbizi ulikuwa wa upande mmoja na bila shaka haukuwa ishara ya kirafiki.

Kurz pia alilizungumzia suala hilo katika mkutano wa Vienna. "Hakujakuwa na uhaba wa mikutano, lakini kumekuwa na uhaba wa ari ya kuzuia wimbi la wakimbizi. Tumekutana leo na sote tunalifanyia kazi lengo moja: Tunataka kupunguza wimbi hili," alisema.

Österreich Deutschland Flüchtlinge bei Passau
Wakimbizi katika daraja linalovuka mto Inn kati ya Ujerumani na Austria Novemba 1, 2015Picha: Reuters/M. Dalder

Kwa kuzingatia lengo hilo washiriki wa mkutano wa Vienna walijadili njia za kuwatambua na kuwasajili wakimbizi, kwa lengo la kuwaruhusu tu wale wanaohitaji kusafiri katikati mwa Ulaya kwa sababu za kiusalama. Katika kutimiza azma hiyo, Austria imeahidi msaada wa polisi kwa Macedonia, na idadi ya maafisa wa polisi walio katika mpaka wa Macedonia itaongezwa kutoka 6 hadi 20.

Ofisi maalumu katika wizara ya mambo ya ndani ya Austria itakayokuwa na kibarua cha kuratibu juhudi za polisi kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaowasafisha binaadamu Ulaya, itafunguliwa Aprili 1 mwaka huu.

Mataifa ya Balkan yaelewa msimamo wa Austria

Kwa ujumla, mawaziri wa mambo ya ndani na ya nje walioalikwa Vienna waliunga mkono mipango ya Austria. "Ikiwa nchi zote zilizochukua wakimbizi mpaka sasa zimefikia ukingoni, basi tuna tatizo kubwa," alisema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Macedonia, Nikola Poposki.

"Kwa sasa tuna wakimbizi wapatao 7,000 wanaotaka kuendelea na safari kwenda Serbia, na takriban watu 5,000 upande wa mpaka wa Ugiriki. Hawako katika hali ya kuhatarisha maisha, lakini kuna shinikizo kubwa kwa Macedonia na tunashukuru kwa msaada wa Austria," alisema.

Waziri wa mambo ya ndani wa Slovenia, Vesna Györkös Znidar, pia aliukosoa Umoja wa Ulaya na Ugiriki na kuunga mkono mtazamo wa Austria. "Eneo la Schengen lazima lifanye kazi katika siku zijazo. Slovenia haiwezi kuwa muhanga wa sera ambazo hazijaratibiwa eneo la kaskazini," alisema.

Griechenland Idomeni Flüchtlingslager
Wakimbizi katika kambi ya Idomeni, UgirikiPicha: Dimitris Tosidis

Waziri wa mambo ya ndani wa Serbia, Nebojsa Stefanovic, alikubaliana naye. "Kama Austria, Ujerumani na Sweden hazitafunga mipaka yao, basi hata sisi hatutaifunga," alisema. "Maboresho ya usajili ni muhimu. Kwanza, ni kazi kubwa, na pili, wakimbizi ambao tayari wameteseka vya kutosha, hawatakiwi kulazimishwa kupitia utaratibu huu katika kila nchi wanayoingia," aliongeza kusema.

Leo mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya wanafanya mazungumzo mapya kuhusu uhamiaji, kutafuta njia za kupunguza wimbi la wakimbizi wanaopitia eneo la Balkan na kupanga kuhusu kile ambacho umoja huo umekieleza kuwa ni janga la kibinaadamu linaloweza kutokea. Mawaziri kutoka nchi ambazo si wanachama wa umoja wa Ulaya - Serbia, Macedonia na Uturuki -zitahudhuria mkutano huo.

Mwandishi:Numanovic, Emir/Vienna

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Ummilkheir Hamidou