Ugonjwa usiojulikana umesababisha vifo vya watu kadhaa DRC
4 Desemba 2024Kwa mujibu wa maafisa wa ngazi za juu wa Kongo, timu ya madaktari imepelekwa katika kitengo maalum cha afya cha Panzi katika jimbo la Kwango ili kuchukuwa sampuli na kuanzisha uchunguzi ili kujaribu kuutambuwa ugonjwa huo.
Taarifa za ugonjwa huo zimetolewa na Naibu gavana wa mkoa wa Kwango, Remy Saki kwa ushirikiano na waziri wa afya wa DRC Apollinaire Yumba ambao wameeleza kuwa vifo hivyo vilitokea kati ya Novemba 10 na 25 mwaka huu, na kwamba watu zaidi ya 100 wamefariki. Yumba amewatolea wito raia kuchukua tahadhari na kujiepusha kuzigusa maiti ili kuepuka kuambukizwa, huku akitoa wito kwa taifa na washirika wa kimataifa kutoa vifaa vya matibabu ili kuushughulikia mgogoro huo wa kiafya.
Dalili za ugonjwa huo ni kukohoa, homa, kuumwa na kichwa
Kulingana na naibu mratibu wa kitengo cha umma kinachojihshughulikia dharura za kiafya Mathias Mossoko, dalili za ugonjwa huo ni kukohoa, homa, kuumwa na kichwa, dalili za mafua, kupata joto kali mwilini na matatizo ya kupumua. Massoko ameahidi kutoa maelezo zaidi juu ya janga hili, mara tu uchunguzi wa maabara utakapokamilika na matokeo kutolewa. Zaidi Massoko anasema " Katika ngazi ya mkoa tunadhani inaweza kuwa nimonia, ugonjwa ambao katika muktadha wautapiamlo, jambo ambalo pia limesababisha vifo vya watoto. Hii ndio taarifa tunayoweza kuwapeni kwa sasa, kutoka hapa katika kituo cha operesheni ya dharura ya Afya ya Umma ya DRC. "
Kiongozi mmoja wa shirika la kiraia Cephorien Manzanza ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hali inatia wasiwasi mkubwa kufuatia kiwingu cha kuongezeka kwa idadi ya walioambukizwa .Mtaalamu mmoja wa magonjwa ya mripuko kwenye eneo hilo amesema wengi walioambukizwa ni wanawake na watoto.
Bado kunahitajika jitihada zaidi katika kunusuru Wakongo kitaalamu
Wakati wakisubiri wagonjwa kushughulikiwa ipasavyo na serikali kuu, mamlaka ya mkoa wa Kwango inaweza kutegemea msaada muhimu kutoka kwa washirika mbalimbali wa Kongo kama anavyoeleza Naibu wa gavana wa jimbo la Kwango Remy Saki." Kuna washirika wa jadi wa DRC ambao wamesaidia kutoa dawa na baadhi ya vifaa vya kinga, hasa UNICEF, WHO na SANRU. Lakini pia kuna wanasiasa wenye nia njema ambao wamechangia fedha ili kupunguza makali ya mzozo huu wa kiafya. Pamoja na mambo mengine, itabidi tutafute njia na mbinu za kuendelea kutoa msaada wa kiufundi na kifedha ili tuweze kudhibiti janga hili."
Soma zaidi:Mkutano mpya wa amani DRC kufanyika Luanda
Kati ya Novemba 10 na Desemba 2, mamlaka ya afya katika jimbo la Kwango imesema waliorodhesha vifo zaidi ya 140. Mkoa huo unapakana na mkoa wa zamani wa Grand Kasaï, ambapo kiwango cha utapiamlo kinaonekana kuwa cha juu. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari inakabiliwa na janga la Mpox, ikiwa na zaidi ya visa 47,000 vinavyoshukiwa na zaidi ya vifo 1,000, hii ikiwa ni kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO.