1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaazimia kupambana na ukeketwaji dhidi ya wanawake

Dinah Gahamanyi7 Aprili 2006

Madaktari nchini Ujerumani wamepitisha miongozo na kanuni za matibabu kwa wanawake walioathirika na ukeketwaji, wakibainisha kuwa ukeketaji dhidi ya wanawake ni kosa la jinai chini ya sheria za Ujerumani na kwamba madaktari wanaowakeketa wanawake wataadhibiwa.

https://p.dw.com/p/CBJ7

Nchini Ujerumani kuna jumla ya wahamiaji wasichana takriban 30,000 na wanawake kutoka Afrika na Uarabuni waliofanyiwa ukeketwaji ni miongoni mwao.

Licha ya kwamba wengi wao walikeketwa miaka kadhaa iliyopita, idadi kubwa ya wanawake hao bado wanapata matatizo ya kiafya kutokana na kitendo hicho kama vile maambukizi sugu , kuvuja damu na hata wakati mwingine husababisha kufa.

Madaktari wa ujerumani kwa kushirikiana na serikali sasa wamepitisha miongozo juu ya namna ya kuwasaidia wanawake hao.

Waziri wa afya nchini ujerumani Ulla shmidt anasema miongoni mwa sera zilizopitishwa ni pamoja na kutokubaliana kabisa na kitendo cha kuwakeketa wanawake.

''Ukeketwaji dhidi ya wanawake ki kinyume kabisa na sheria za Ujerumani.

Lakini tunamatumaini kuwa tutaweza kuwafahamisha madaktari wa ujerumani juu ya tatizo hili na zaidi tutajitahidi kubadilisha mtizamo baina ya wanawake hawa na familia zao kwa kuwapatia ushauri.'' Alisema Ulla Schmidt.

Katika miongozo yao madaktari wa Ujerumani kwanza kabisa inabainisha wazi kwamba ukeketwaji dhidi ya wanawake ni kosa la jinai, na inasema madaktari watakaobainika kufanya kitendo hicho watanyang’anywa vibali vya kazi yao na kushtakiwa kwa kuhatarisha mwili.

Wanawake wanakabiliwa na matatizo ya kiafya kutokana na ukeketwaji, hata hivyo watapatiwa ushauri nasaha wa kitaaluma kwa gharama zitakazolipwa kwa bima ya matibabu .

Hii ni pamoja na kupatiwa dawa, kusaidiwa kisaikolojia na vile vile mkalimani, ili kuwasaidia wanawake kuelewa uhusiano wa matibabu anayopatiwa na ukeketwaji.

Mwongozo huo wa madaktari wa Ujerumani ni sehemu ya kampeni ya dunia dhidi ya ukeketwaji wa wanawake.

Waris Dirie, mzaliwa wa Somalia, ambaye pia alikeketwa mwanaharakati wa umoja wa mataifa aliyejitolea kupiga vita ukeketwaji anasema ni muhimu kuwapatia wanawake na familia kwa ujumla uelewa juu ya athali za ukeketwaji.

``NI vigumu kubadili mawazo ya watu na wanafikiri namna wanavyofanya katika maisha yao. Ndio maana wanahitaji kueleweshwa, wanahitaji elimu, wanahitaji vyanzo vyote vya habari kadiri iwezekanavyo.’’ Alisema Waris Dirie.

Serikali ya ujerumani inatumia fedha zinazoweza kupatikana katika kampeni na chini ya utawala wa Kansela Angela Merkel vita dhidi ya ukeketwaji wanaofanyiwa wanawake ni miongoni mwa kampeni zinazonufaika na misaada ya Ujerumani kwa nchi za nje.

Jumla ya wasichama milioni 135 na wanawake duniani wamefanyiwa ukeketwaji hususan kutoka Afrika na nchi za kiarabu na baadhi yao sasa wanaishi katika nchi zilizoendelea ambako madaktari wanajiuliza ni namna gani watakavyopata dawa za matibabu dhidi ya vitendo hivyo vya kimila walivyofanyiwa.