1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yahitaji wanawake katika nafasi za uongozi

18 Oktoba 2011

Magazeti ya Ujerumani leo hii yamezungumzia zaidi kuhusu nafasi sawa za kazi kwa wanawake na wanaume.Halikadhalika suala la mzozo wa madeni katika eneo la mataifa yanayotumia sarafu ya euro.

https://p.dw.com/p/12uCG

Magazeti ya Ujerumani hii leo yamezungumzia zaidi kuhusu nafasi sawa za kazi kwa wanawake na wanaume nchini Ujerumani, halikadhalika suala linalogonga vichwa vya habari kila siku la mzozo wa kiuchumi katika eneo la mataifa yanayotumia sarafu ya euro na mzozo wa mabenki.

Tuanze na gazeti la Stuttgarter Nachrichten likizungumzia kuhusu kuwapo na kiwango maalumu cha wanawake katika uongozi wa nchi na makampuni hapa Ujerumani. Gazeti linaandika.

Nafasi sawa za kazi wanazipata wanawake pale tu wanapobaki bila ya kuwa na mtoto. Na msingi wa kupanda ngazi katika kazi unatokea wakati mtu akiwa na umri wa kati ya miaka 30 hadi 40, na kama mwanamke ambaye anajiamini na anataka kupiga hatua, kuna uwezekano wa kupitwa pia. Mahakama ya Ujerumani mwezi Agosti ilifikia uamuzi, kuwa mama ambaye ni mzazi anayelea peke yake watoto wake anapaswa kuchukua jukumu la ulezi huo binafsi. Na hapa kila mwanamke wa pili ambaye ameachika, ana hatari ya kupoteza sio tu kazi yake, bali pia kuna hatari ya kuathirika katika mapato yake, iwapo atataka kujenga familia yake. Suala la kuwa na idadi maalum ya wanawake katika uongozi inaweza kulazimisha kisiasa na kiuchumi kujaribu kuliweka katika hali bora zaidi suala la ulezi. Wanawake hawahitaji zaidi ya msaada, ili kuendelea na kazi zao.

Gazeti la Braunschweiger Zeitung, likizungumzia kuhusu mada hiyo linaandika.

Mbinyo kutoka chini na juu lazima uongezeke, ili katika miaka ijayo tuweze kuona hali bora zaidi. Kwa hiyo ukweli ni kwamba, makampuni yaamue binafsi kuajiri viongozi wengi zaidi wanawake kama sehemu ya kuinua hadhi yao. Yule ambaye atashindwa kujiangalia kwa ndani, atapoteza uaminifu. Pia ukweli ni kuwa kuna hali inayoongezeka ya kupungukiwa na wafanyakazi wenye ujuzi. Enzi ya uchumi unaoongozwa na wanaume peke yao inafikia mwisho, hata katika kampuni la soko la hisa la DAX na hii ni bila ya kuwapo sheria maalumu inayoelekeza hivyo.

Suala la mzozo wa mabenki na kiuchumi katika umoja wa sarafu ya euro pia limezungumziwa na wahariri wa magazeti ya leo. Gazeti la Der neue Tag kuhusu mzozo wa madeni linaandika.

Kwa kutoa wito baada ya mabenki kupata matatizo ya kifedha, kiongozi wa chama cha upinzani cha SPD, Sigmar Gabriel, na wenzake wote wale walioonyesha wasiwasi wao , wamechelewa kwa muda wa miaka mitatu sasa . Mwishoni mwa mwaka wa 2008 wakati mzozo wa kiuchumi ukilikumba bara la Ulaya, hatua hii ilipaswa kuelezwa, kuhusiana na ulazima wa kuyapatia mitaji mabenki. Badala yake umepotea muda mrefu. Na sasa hatua hiyo itakuwa ghali sana kwa mabenki na hususan walipa kodi.

Nalo gazeti la Handelsblatt linalochapishwa mjini Düsseldorf, kuhusiana na mkutano unaotarajiwa kuzungumzia suala la uokozi kwa nchi zenye madeni, linaandika.

Kulikuwa wakati fulani katika mkataba wa umoja wa Ulaya marufuku ya kuokoa nchi zenye madeni. Miaka miwili baada ya kuzuka kwa mzozo wa nchi zenye madeni katika bara la Ulaya hii ilionekana kama kupitia katika enzi za kale. Lakini kifungu cha 125 cha mkataba wa Lisbon inaonekana kimebadilishwa. Serikali ya mseto ya Ujerumani haichukulii hali hii kuwa ni lazima kwa mataifa wanachama. Lakini gazeti linauliza msimamo huu una maana yoyote kisiasa ?

Je, serikali za mataifa ya eneo la euro yameamua kuwa chochote kinawezekana, hata kama wanaukiuka mkataba? Siku utakapofanyika mkutano ujao ambao kwa hakika si wa mwisho kuhusu mzozo wa eneo la euro, suali hili litakuwa linauzingira mkutano huo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse/ Stuttgarter Nachrichten, Braunschweiger Zeitung, Der neue Tag , Handelsblatt.

Mhariri: Josephat Charo.