Kansela Scholz apoteza kura ya imani bungeni
17 Desemba 2024Wabunge 394 kati ya 717 wa Bunge la Taifa, Bundestag, walipiga kura ya kutokuwa na imani na serikali ya Scholz huku 207 pekee ndiyo walimuunga mkono. Kufuatia matokeo hayo Scholu alimwomba Rais Frank-Walter Steinmeier kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi.
Kura hiyo ya imani bungeni inafuatia kusambaratika kwa serikali ya mseto Kansela Scholz baada ya kiongozi huyo kumfuta kazi waziri wake wa fedha kutoka chama mshirika cha FDP kutokana na mabishano juu ya namna ya kufadhili bajeti ya mwaka ujao.
Uamuzi huo wa mwezi Novemba uliiweka rehani serikali ya Scholz anayetoka chama cha SPD na washirika wengine wa chama cha kijani, Die Grüne.
Uchunguzi wa maoni ya umma unaonesha umashuhuri wa Scholz umeporomoka na kuna uwezekano mkubwa kwa chama cha kihafidhina cha CDU cha Kansela wa zamani Angela Merkel kurejea madarakani.