Ulaya yalaumiwa kurejesha kwa nguvu waomba hifadhi
5 Oktoba 2017Mataifa ya Ulaya yanawarejesha nyumbani raia wengi wa Afghanistan wanaoomba hifadhi kwenye nchi hizo, wakati ambapo machafuko kwenye nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita yakiongezeka, hii ikiwa ni kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na shirika la utetezi wa haki za binaadamu la Amnesty International iliyotolewa Alhamisi hii (05.10.2017).
Shirika hilo la utetezi wa haki za binaadamu limesema serikali za Ulaya zimeendelea kufumbia macho hatari inayowakabili raia wanaorejeshwa, huku Umoja wa Ulaya ukiishinikiza kwa nguvu Afghanistan kupokea idadi kubwa ya watu hao wanaorejeshwa.
Kuanzia mwaka 2015 hadi 2016, idadi ya raia wa Afghanistan waliorejeshwa nchini mwao kutoka Ulaya iliongezeka kiasi mara tatu kutoka 3,290 hadi 9,460. Idadi hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya Amnesty, ikirejelea takwimu ya Umoja wa Ulaya.
Wakati huohuo, idadi ya raia waliojeruhiwa imebakia kuwa juu, wakati watu 11,418 waliuawa ama kujeruhiwa mnamo mwaka 2016, idadi ambayo imetolewa na ujumbe wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan. Idadi hiyo imepanda kutoka 11,002 ya majeruhi ya raia mwaka 2015, kulingana na ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa, UNAMA.
Amnesty imetoa mwito wa kusitishwa kwa mpango huo wa kurejeshwa kwa raia hao hadi pale nchi hiyo itakapokuwa mahala patakapofaa kwa "usalama na utu".
"Katika kufikia azma yao ya kuongeza idadi ya watu wanaorejeshwa makwao, serikali za Ulaya zinatekeleza sera isiyozingatia madhara ya mbeleni na iliyo kinyume cha sheria", amesema mtafiti wa haki za wakimbizi na wahamiaji kutoka shirika hilo la Amnesty International Anna Shea, kwenye taarifa yake. Kuufumbia macho kwa makusudi ushahidi kwamba bado kuna machafuko ya kutisha nchini humo na hakuna sehemu ambayo iko salama, ni kuwaweka watu katika hatari ya mateso, utekwaji, vifo na hata hofu".
Ripoti hii imejikita kwenye utafiti uliofanywa ndani na kwenye maeneo ya matukio kati ya mwezi Mei na Septemba 2017 na kuweka kumbukumbu ya visa jumla 26.
Afghanistan imepitia mateso ya miongo minne iliyogubikwa na machafuko makubwa na miaka 16 ya vita ambayo ilianza kwa uvamizi wa Marekani mwaka 2001 yaliyolenga kuwasaka waliohusika na mashambulizi ya Septemba 11. Raia wa kawaida wa Afghanistan wanafadhaishwa na unyanyasaji huo, pamoja na kushindikana kwa hatua za kuwaweka salama na kupata amani.
Taasisi za kiusalama zinaripoti kuwa angalau makundi 20 ya wanamgambo, ambayo ni pamoja na Taliban na kundi lenye mashikamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS bado yanaendeleza mashambulizi nchini Afghanistan, na hususan kwenye maeneo ya mipaka karibu na Pakistan.
Kati ya mwaka 2009 na 2016, UNAMA ilisema takriban raia 25,000 waliuawa na zaidi ya 45,000 walijeruhiwa. Machafuko hayo, pamoja na kuzorota kwa usalama yameendelea kujitokeza mwaka huu.
Mnamo mwezi Agosti, wanamgambo waliuvamia msikiti uliofurika waumini wa Kishia mjini Kabul wakati wa swala ya Ijumaa, na kusababisha vifo vya watu takriban 20, na wengine 50 kujeruhiwa vibaya. Mei 31, katika moja ya mashambulizi makubwa katika historia ya Kabul, zaidi ya watu 150 waliuawa na wengi zaidi kujeruhiwa wakati bomu liliporipuka karibu na eneo lenye balozi za Umoja wa Ulaya, ambalo ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na ulinzi mkali zaidi katika mji huo mkuu wa Afghanistan.
Kulingana na ripoti hiyo, nchi tano za Ulaya zilizorejesha idadi kubwa ya Waafghanistan mwaka 2016, zilikuwa ni Ujerumani iliyorejesha raia 3,440, ikifuatiwa na Ugiriki, Sweden, Uingereza na Norway. Aidha, ripoti hiyo imegundua kwamba, Norway, imeonekana kuwa moja ya nchi za Ulaya ambayo imerejesha idadi kubwa ya raia hao kwa nguvu.
Shirika hilo limerejelea mamlaka ya Afghanistan na kusema, miongoni mwa raia hao waliorejeshwa kwa nguvu katika miezi ya minne ya mwanzo wa mwaka huu, asilimia 32 walitokea nchi hiyo iliyoko Kaskazini mwa Ulaya.
Mwandishi: Lilian Mtono/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga