EU yatangaza makubaliano ya kibiashara na Amerika Kusini
6 Desemba 2024Rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema katika taarifa kuwa, makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya EU na Mercosur ni “mkataba wa ushindi kwa pande zote mbili.”
"Ngoja niwaeleze wenzangu wa Umoja wa Ulaya. Mkataba huu ni ushindi kwa Ulaya. Makampuni 60,000 yanasafirisha bidhaa zao leo kwenda Mercosur, 30,000 kati ya hayo ni makampuni madogo na ya kati. Wanafaidika na kupunguzwa kwa ushuru, taratibu nyepesi za forodha na upatikanaji wa baadhi ya malighafi muhimu. Mkataba huu utabuni fursa kubwa za biashara."
Makubaliano hayo ya biashara huri yanahusisha zaidi ya watu milioni 700, na kuyafanya kuwa mojawapo ya maeneo makubwa zaidi ya biashara huria duniani na yanazijumuisha Brazil, Argentina, Paraguay, Uruguay.
Bolivia ambayo ni mwanachama mpya wa Mercosur na Venezuela ambayo ilisimamishwa uanachama wake tangu mwaka 2016 hazijajumuishwa kwenye makubaliano hayo.