1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yalia na mauaji kiholela ya raia Yemen

28 Desemba 2017

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeua raia 109 katika mashambulizi tofauti ya ndege katika kipindi cha siku 10, wakiwemo 54 katika soko lenye shughuli nyingi na 14 wa familia moja waliokuwa shambani.

https://p.dw.com/p/2q3mS
Jemen - Luftangriffe bei Saana
Picha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Jamie McGoldrick ameyaeleza mapigano yanayoendelea nchini humo kuwa yasiofaa na ya kuhuzunisha, katika ukosoaji usio wa kawaida wa moja kwa moja wa vita ambamo muungano huo, unaoungwa mkono na Marekani, Uingereza na mataifa mengine, unapigana dhidi ya vuguvugu la kabila la Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Ikitaja ripoti za awali kutoka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, taarifa ya mcgoldrick imesema mashambulizi hayo ya ndege yalililenga soko lenye watu wengi katika wilaya ndogo ya Al Hayma katika mkoa wa Taiz siku ya Jumanne, na kuuwa watu 54 na kuwajeruhi 32. Nane kati ya waliokufa na sita miongoni mwa majeruhi walikuwa watoto kulingana na ripoti hizo.

Katika siku hiyo hiyo, shambulizi la ndege kwenye shamba lililopo wilaya ya Attohayta katika mkoa wa Hodeidah liliuwa watu 14, na mashambulizi ya ndege kwingineko yakauwa raia wengine 41 na kuwajeruhi 43 katika kipindi cha siku 10.

Houthis tragen die Leiche eines Mannes, der durch Luftangriffe in ein von Houthi geführtes Haftzentrum in Sanaa getötet wurde
Wahouthi wakibeba maiti ya mmoja ya wahanga wa shambulio la ndege za muungano mjini Sanaa.Picha: Reuters/K.Abdullah

Vita visivyofaa na vya kuhuzunisha

"Matukio haya yanadhihirisha kutojali kabisaa maisha ya watu ambako pande zote, ukiwemo muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, yanaendelea kuonyesha katika vita hivyo vya kuhuzunisha, ambavyo vimesababisha tu uharibifu wa nchi na mateso yasiostahili ya watu wake, ambao wanaadhibiwa kama sehemu ya kampeni ya kijeshi isiyofaa kwa pande zote mbili," alisema McGoldrick katika taarifa yake.

Chini ya sheria ya kimataifa, pande zinazohasimiana laazima ziwaachilie raia pamoja na miundombinu ya kiraia. Umoja wa Mataifa hauna makaridio ya karibuni zaidi kuhusu idadi ya vifo nchini Yemen, baada ya kusema Agosti 2016, kwamba kwa mujibu wa vituo vya afya watu wasiopungua 10,000 wameuawa.

Umoja wa Mataifa unasema mgogoro wa Yemen ndiyo mbaya zaidi wa kibinadamu, ambapo watu wapatao milioni nane wako katika hatari ya kukubw ana janga la njaa, mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliowaathiri watu milioni moja, na mporomoko wa uchumi katika nchi ambayo tayari ilikuwa moja ya mataifa maskini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu.

Mgogoro wa Yemen ulishika makali Machi 2015, wakati waasi wa Kihouthi waliposonga mbele kuelekea mji mkuu wa muda wa serikali wa Aden, na kuilaazimu Saudi Arabia pamoja na mataifa washirika ya Kisunni kuanzisha kampeni ya mashambulizi ya ndege dhidi ya kundi hilo la Kishia. Saudi Arabia inahofu kwamba waasi hao wataipa Iran nafasi ya kuongeza ushawishi wake katika rasi ya Arabia.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae,rtre.

Mhariri: Daniel Gakuba