Urusi yarefusha kibali cha Snowden hadi 2020
18 Januari 2017Msemaji wa ya mambo ya nchi za nje Maria Zakharova ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kibali cha kusihi cha Snowden kimerefushwa "hadi 2020".
Awali, msemaji huyo kupitia ukurasa wa Facebook alisema kibali cha Snowden kiliongezwa kwa miaka miwili, huku akitumia yanayoweza kuwa na utata kwa lugha ya Kirusi.
Wakili wa Snowden, mrusi Anatoly Kucherena amethibitisha taarifa hizo kwa shirika la habari la RIA Novosti, kwamba idara ya uhamiaji ya Urusi mapema mwezi huu iliongeza muda wa kibali cha mteja wake kuishi kwa miaka mitatu baada ya kukaa nchini humo kwa miaka mitatu hadi sasa.
Wakili huyo ameongeza kwamba ikiwa Snowden ataishi Urusi kwa miaka mitano, atakuwa na uwezo wa kuomba uraia wa kudumu, "hilo linawezekana katika siku za usoni."
Mkandarasi huyo wa zamani wa shirika la usalama aliishtuwa taasisi ya usalama ya Marekani mwaka 2013 kwa mlolongo wa uvujaji wa taarifa za ukaguzi mkubwa ndani ya Marekani na duniani kote.
Tangazo la Urusi linakuja wakati rais Barack Obama akiwa amepunguza adhabu ya mwanajeshi Chelsea Manning ambaye alifungwa miaka 35 jela kwa kuvujisha taarifa za siri za Marekani kwa mtandao wa Wikileaks.
Snowden hakuwepo katika orodha ya Obama ya waliosamehewa au kupunguziwa adhabu. Amekuwa akiishi uhamishoni Urusi tangu mwaka 2013 baada ya kuishi mafichoni kwa wiki tatu katika uwanja wa ndege wa Urusi wa Sheremetyevo.
Mwanzoni alipewa hifadhi ya mwaka mmoja na Urusi wakati mahusiano baina ya Moscow na Washington yalipozorota.
Wakili wake anasema Snowden amekuwa na maisha mazuri na akiendelea na shughuli zake ikiwemo kusafiri na kufanya kazi.
Hata hivyo hajaonekana hadharani nchini Urusi tangu kuwasili kwake ingawa amefanya mahojiano mara mbili akiwamaeneo ya siri.
Ushahidi uliopatikana katika nyaraka alizovujisha kulisababisha wasiwasi mkubwa wa taarifa zinazokusanywa na Marekani ndani ya nchi na washirika wake wakiwemo viongozi wake.
Snowden mwenyewe ameukaribisha uamuzi wa Rais Obama wa kumsamehe Manning, akisema kupitia ukurasa wake wa Twitter, "wacha isemwe hapa kwa bidii na nia njema, asante Obama".
Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa Snowden kufuatia uamuzi wa Obama, msemaji wa Ikulu ya Urusi Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia wanahabari kuwa hilo sio suala la Kremlin kwasababu hawana taarifa ya nini alifanyalo Snowden.
Mawasiliano yoyote na Snowden ni kupitia kwa mawakili wake wa Urusi na Marekani, aliongeza Peskov. Kaimu Mkurugenzi wa zamani wa CIA Michael Morell katika maoni yake wiki hii alipendekeza kwamba Putin anaweza kumkabidhi Snowden kuashiria utawala wa Donald Trump.
Hata hivyo Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi Zakharova amelilaani pendekezo la Morell kutaka wale kuwakabidhi wale wanaotafuta kinga na kuongeza kwamba Morell bado haielewi Urusi,.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi /AFP
Mhariri: Mohamme Abdul-Rahman