Vifo Gaza vyaongezeka hadi 77 tangu makubaliano yalipofikiwa
16 Januari 2025Mashambulizi ya angani yamewauwa watu 77 huko Gaza, saa chache baada ya mpango wa kusitisha mapigano na kuwaachia mateka kutangazwa.
Wizara ya afya ya Gaza imesema watu 81 wameuawa katika saa 24 zilizopita na karibu 188 wamejeruhiwa. Shirika la Huduma za Dharura la Kipalestina limesema watu 77 kati ya hao waliuawa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipotangazwa.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa jana baada ya upatanishi wa Qatar, Misri na Marekani.
Misururu ya malori ya misaada yamejipanga katika mji wa mpakani wa Misri wa El-Arish yakisubiri kuvuka hadi Gaza, mara tu mpaka utakapofunguliwa tena.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amechelewesha mkutano wa baraza lake la mawaziri uliopangwa kufanyika Alhamisi kwa ajili ya kuidhinisha makubaliano hayo.
Ameishutumu Hamas kwa kuweka masharti ya dakika za mwisho mwisho kwenye makubaliano hayo.
Hata hivyo afisa mwandamizi wa Hamas Izzat el-Reshiq amesema kundi hilo limedhamiria kuheshimu mpango huo.