1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

'Vikombe maalum' vya hedhi kuwasaidia kina mama Kenya

Wakio Mbogho10 Januari 2020

Shirika la Hope in Life nchini Kenya limeanza kuwahamasisha kina mama namna ya kutumia 'vikombe maalum' vya hedhi. Vikombe hivyo vinaweza kutumiwa kwa muda wa masaa 12 kwa wakati mmoja.

https://p.dw.com/p/3W0Mt
Miongoni mwa wadau waloshiriki mradi wa kuwahamasisha wasichana na wanawake kutumia 'vikombe maalum' vya kusaidia wakati wa hedhi.
Miongoni mwa wadau waloshiriki mradi wa kuwahamasisha wasichana na wanawake kutumia 'vikombe maalum' vya kusaidia wakati wa hedhi.Picha: DW/W. Mbogo

Shirika moja la Hope in Life la mjini Nakuru Kenya limezindua mpango wa kusambaza na kuhimiza matumizi ya vikombe maalum vitakavyotumika na akina mama wakati wa hedhi, kama njia mojawapo ya kukabiliana na maradhi pamoja na kupunguza gharama kwa wanawake wasioweza kumudu taulo za hedhi kila mwezi.

Akizungumzia kifaa hicho, Mary Muthoni ambaye ni miongoni mwa kina mama vijana walioshawishika kukitumia kifaa hicho amekiri kuwa hapo mwanzoni alikiona kifaa hicho cha hedhi kama jambo geni, lakini sasa amebadili mtizamo wake.

Kifaa hicho kilicho na muundo kama chombo cha kukingia mafuta katika chupa kimetengezwa kwa aina ya mpira laini silikoni. Mtumiaji anahitajika kukisafisha bila kutumia dawa za kuua viini kila anapokitumia. Muthoni ameeleza zaidi kuwa mwanamke anaeweza kukitumia hadi muda wa masaa 12 kwa wakati mmoja, na ni salama kutumiwa usiku na mchana. Kila kifaa kinaweza kutumika kwa zaidi ya miaka kumi, hivyo kinamfaa mtu mwenye kipato cha chini. Shirika la Hope in Life kwa ushirikiano na wakfu wa Sulwe wameanzisha mradi wa kutoa mafunzo na kusambaza kifaa hicho cha hedhi kwa kina mama wachanga hasa wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.

Miongoni mwa walioshiriki mkutano wa kuwahamasisha wanawake namna ya kutumia vikombe hivyo maalum vya hedhi mjini Nakuru Kenya.
Miongoni mwa walioshiriki mkutano wa kuwahamasisha wanawake namna ya kutumia vikombe hivyo maalum vya hedhi mjini Nakuru Kenya.Picha: DW/W. Mbogo

"Kipindi cha hedhi ni kizuizi kikuu kwa maendeleo kwa wanawake kutoka jamii zisizojiweza. Tumeamua kuwapa vifaa hivi kuwawezesha kuyaendeleza maisha yao kama kawaida. Tunalenga kuwafikia wote wanaojitaji popote walipo." Amesema daktari Pius Sulwe, afisa mkuu katika wakfu huo anaeleza.

Mradi huu umepata uungwaji mkono na serikali ya Kenya, na kama Daktari Torome Kochei kutoka wizara ya afya ambaye ameutaja kuwa mradi wa kipekee ambao utasaidia sana kukabiliana na maradhi kwa wanawake.

Kikao(kifaa) hiki ni cha kipekee, tunaangazia usafi wa kina mama wasiojiweza ambao huenda wasimudu hizo njia zingine kwa sababu kama wizara ya afya hatutibu tu bali pia tunahimiza kuepukana na maradhi. Ameeleza Dkt. Torome.

Suala la uwezo wa watu wenye mapato ya chini kupata taulo za hedhi ni kero kuu kwa jamii nyingi nchini Kenya, ndiposa serikali inahimiza mikakati itakayoangazia upungufu huu na hatimaye kutoa suluhu.