Vikwazo vya Marekani na Madhara yake Magazetini
7 Agosti 2018Tunaanza na uamuzi wa Marekani wa kuiwekea upya Iran vikwazo vya kiuchumi baada ya rais Donald Trump kuitoa nchi hiyo katika makubaliano ya kimataifa kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran. Ni uamuzi wa upande mmoja lakini madhara yake yanatishia makampuni ya nchi nyengine pia linaandika gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung": "Juhudi na bidii zilihitajika hadi makubaliano hayo yalipofikiwa. Rais Trump ameyavunja akihoji si makubaliano ya maana. Matokeo yake yanabainisha madaraka ya aina gani anamiliki kiongozi huyo anaependa kutumia jukwaa la Twitter kuwakaripia walimwengu.
Kwasababu vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vitayaathiri makapuni ya nchi nyengine pia.Cha kutegemewa ni kusubiri na kuona kama Umoja wa Ulaya hautakubali kutishwa na Marekani. Sheria iliyopewa jina "Blocking Statute" inayoyazuwia mataifa wanachama kufuata vikwazo vya Marekani ni hatua ya maana. Pindi Umoja wa Ulaya ukibadilisha msimamo wake, hali hiyo itailetea madhara makubwa Iran na wakati huo huo kudhoofisha ushawishi wa nchi za Umoja wa Ulaya mazungumzo ziada yakiitishwa siku za mbele."
Nguruma za simba hazimtishi Chui
Gazeti la "Mannheimer Morgen" linasifu msimamo wa Umoja wa Ulaya na kuandika: "Maneno yanabainisha ujasiri wa Umoja wa Ulaya. Wataendelea kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa kwa wakati wote ambao Teheran nayo itayaheshimu. Si hayo tu wamefika hadi ya kuifufua ile sheria inayojulikana kama Blockade Statute. Sheria hiyo inayakataza makampuni ya nchi za umoja wa ulaya kufuata amri kutoka Marekani. Ni sawa na simba anaenguruma ingawa ngurumo hizo safari hii zitakuwa na athari kwa wengine: shughuli za kiuchumi. Umoja wa Ulaya hautoweza kuyanusuru makampuni mengi dhidi ya ghadhabu za Trump, kwasababu kwao wao biashara pamoja na Marekani ni muhimu zaidi kuliko ile pamoja na Iran."
Jinsi ya kuwalinda watoto wasishawishiwe na itikadi kali
Mjadala umepamba moto tangu idara ya upelelezi ilipopendekeza wachunguzwe kwa karibu zaidi watoto wa familia zinazofuata itikadi kali ya dini ya Kiislam. Idara za upelelezi zinahofia watoto hao wasije wakafundishwa pia itikadi kali na wazee wao. Maoni yanatofautiana kuhusu suala hilo, kuna wahariri wanaohisi watoto hao ni wahanga na wengine wanaosema ingekuwa bora kama wasingeruhusiwa kabisa kurejea Ujerumani. Gazeti la "Allgemeine Zeitung" linaandika: "Watoto, waliofundishwa itikadi kali na kusajiliwa na wanajihadi ni wahanga. Ili kuzuwia hali hiyo na hasa kwakua ustawi wa watoto unabidi utangulizwe mbele, basi litakuwa jambo la maana kama idara za usalama zitakuwa na uangalifu mkubwa mbele ya watoto hao kwa lengo la kuwanusuru wasiangukie mikononi mwa makundi ya itikadi kali."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga