Viongozi wa SADC wajadili ghasia za uchaguzi Msumbiji
19 Desemba 2024Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, amewaeleza waandishi wa habari kuwa Rais Cyril Ramaphosa anashiriki mazungumzo na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji.
Soma pia: Mzozo wa kisiasa wa Msumbiji kutawala mkutano wa kilele wa SADC
Ronald Lamola alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na waandishi wa habari, akiongeza kuwa hawatatoa taarifa zozote kuhusu mazungumzo hayo hadi Baraza la Katiba la Msumbiji litakapokamilisha mchakato wa uhakiki wa kura, kufuatia madai ya uwezekano wa ulaghai katika uchaguzi wa Oktoba 9.
Michakato yote italazimika kusubiri matokeo ya Baraza la Katiba ikiwa kutakuwa na matangazo yoyote yatakayotolewa.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri Lamola aliandamana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji, Pascoal Ronda, ambaye alithibitisha kuwa Rais wa Msumbiji alijaribu kumtafuta kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, kwa mazungumzo ya kutafuta suluhisho, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa.
Soma pia: Kiongozi wa upinzani Msumbiji aweka masharti ya mazungumzo ya baada ya uchaguzi
Rais wa Msumbiji ametoa mwaliko wa mazungumzo kwa kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane, lakini kwa bahati mbaya, hakuweza kujitokeza.
Katika matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9, mgombea wa Frelimo, Daniel Chapo, alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 71 ya kura, huku Venancio Mondlane, mchungaji wa kanisa na mgombea huru baada ya kujitenga na chama kikuu cha upinzani cha Renamo, akipata asilimia 20 tu. Mondlane alipinga matokeo hayo akidai kuwa kura ziliibwa, na akatoa wito wa maandamano.
Tume ya Uchaguzi ilikanusha madai ya Venancio Mondlane kwamba kura zilichakachuliwa kwa manufaa ya Frelimo, chama ambacho kimekuwa madarakani tangu Msumbiji ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ureno miaka 49 iliyopita.
Je, kushindwa kwa kiongozi wa upinzani kuitikia mwaliko wa mazungumzo kunaipeleka wapi Msumbiji? Hilo ndilo swali nililomuuliza Samson Chars, mchambuzi wa siasa za Afrika akiwa Dar es Salaam, Tanzania.
Takriban waandamanaji 18 na polisi mmoja wamepoteza maisha katika majuma kadhaa ya ghasia nchini Msumbiji, huku baadhi ya mipaka inayounganisha nchi hiyo na Afrika Kusini ikifungwa. Chama cha Usafirishaji wa Barabarani kimeripoti kuwa hali hiyo inagharimu uchumi wa Afrika Kusini takriban dola 548,345 kila siku.