1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wakubaliana wahamiaji kuondolewa Libya

Caro Robi
30 Novemba 2017

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na wa nchi za Umoja wa Afrika wanaokutana katika mkutano wa kilele nchini Ivory Coast wamekubaliana kuhusu mpango wa kuondoa nchini Libya wahamiaji wanaokabiliwa na mateso.

https://p.dw.com/p/2oVTm
Elfenbeinküste EU-Afrika-Gipfel in Abidjan
Picha: Reuters/P. Wojazer

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara katika mkutano wa tano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na wa nchi za Umoja wa Afrika kutoa wito wa hatua za dharura kuchukuliwa kukomesha biashara ya utumwa na mateso mengine dhidi ya wahamiaji yanayoendela Libya. Rais Ouattara amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya kila liwezekanalo kukomesha madhila wanayopitia wahamiaji.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyeongoza kikao cha dharura pembezoni mwa mkutano huo kujadili suala hilo la biashara ya utumwa Libya, amesema viongozi wa Libya, Ujerumani, Chad, Niger, Ufaransa pamoja na nchi nyingine nne na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wameamua kuanzisha operesheni ya dharura kuwaondoa wahamiaji hao kutoka Libya.

Libya yakubali wahamiaji kuondolewa

Waziri mkuu wa Libya Fayez Sarraj amekubali kuruhusu shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM kuingia katika kambi za wakimbizi nchini mwake katika juhudi za kusaidia kuwarejesha makwao wakimbizi hao.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wafanya mazungumzo na Rais wa Ivory Coast Alassane Outtara katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika mjini Abidjan
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ivory Coast Alassane OuttaraPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito kwa Umoja wa Afrika kuyashirikisha makundi yote nchini Libya kwani waziri mkuu Serraj hana mamlaka katika maeneo yote ya nchi hiyo.

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na mwenyekiti kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahmati wametaka hatua za pamoja kuchukuliwa kulishughulikia tatizo hilo. Tusk amesema huu sio wakati wa kulaumiana bali wa kushirikiana ili kuyaokoa maisha.

Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa umetangaza kuanzishwa kwa kikosi cha pamoja cha kuwaokoa na kuwalinda wahamiaji hasa ndani ya Libya na kwa ushirikiano na maafisa wa Libya, kikosi hicho kinalenga kuharakisha kurejeshwa kwa hiari wahamiaji katika nchi zao, kupewa hifadhi kwingineko kwa wanaohitaji ulinzi wa kimataifa, kuyavunja makundi ya wafanyabiashara ya kusafirisha watu kimagendo na magenge ya wahalifu.

Mateso, ubakaji na utumwa Libya

Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari ameapa kuwarejesha nyumbani Wanigeria wote waliokwama Libya na kwingineko duniani.

Wanawake wawili wakimbizi kutoka Nigeria wakikumbatiana na kulia katika kambi ya kuwazuia wakimbizi ya Surman nchini Libya mnamo tarehe 178 mwezi agosti, 2017
Wakimbizi kutoka Nigeria wakilia katika kambi ya wakimbizi LibyaPicha: picture alliance/AP Photo/D. Etter

Mapema mwezi huu, kituo cha televisheni cha CNN kilionesha video inayoaangazia ukiukaji wa haki za binadamu Libya ambako wahamiaji wa Kiafrika waliuzwa mnadamani kama watumwa kwa kiasi cha hadi dola 400.

Kulingana na ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu, wahamiaji wanaozuiwa Libya pia wanateswa, kubakwa na kuuawa.

Suala hilo limeghubika mkutano huo wa Abdijan ulioanza jana na kutarajiwa kukamilika leo. Ajenda kuu za mkutano huo wa Abidjan ni maendeleo kwa kuwekeza kwa vijana, uhamiaji na usalama.

Mkutano huo unalenga kuimarisha viwango vya elimu na fursa za kiuchumi kwa idadi ya watu inayokua kwa kasi barani Afrika ambapo inakadiriwa itaongezeka maradufu hadi watu bilioni 2.4 ifikapo mwaka 2050.

Umoja wa Ulaya unatumai kwa kulisaidia bara la Afrika kujiinua kiuchumi, kutapunguza idadi ya watu wanaotaka kuhamia Ulaya.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Gakuba, Daniel