Vyama vya sera kali za mrengo wa kulia vyakutana Ujerumani
21 Januari 2017"Tunashuhudia kumalizika kwa mfumo wa dunia wa zamani na kuzaliwa kwa mwengine mpya " Marine Le Pen kiongozi wa chama cha sera kali za mrengo wa kulia National Front cha Ufaransa amewaambia wafuasi wa vyama vya sera kali za mrengo wa kulia vyenye kupinga wahamiaji.
Le Pen amemshutumu Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye amepongezwa kila mahala duniani kwa uamuzi wake wa kuruhusu mamia kwa maelfu ya wahamiaji kuingia nchini hapo mwaka 2015.
Len Pen katika mkutano wake wa kwanza wa hadhara nchini Ujerumani amesema "Lakini hakuna mtu aliwauliza Wajerumani wanafikiri nini juuu ya sera hii ya wahamiaji."
Merkel hivi sasa yuko kwenye shinikizo wakati hali ya kukata tamaa ikiongezeka miongoni mwa wapiga kura ambao wamemshutumu kwa namna alivyoushughulikia mzozo huo wa wakimbizi.
Ni mwaka wa kuamka
Le Pen ambaye anatarjiwa kugombea urais nchini Ufaransa ameulezea mwaka 2017 kuwa "ni mwaka wa kuamka kwa watu wa Ulaya ya kati."
Ameongeza wafuasi wa sera za kizalendo hawako tena pembeni na hivi sasa watajipanga kushinda wingi wa viti katika uchaguzi mwaka huu nchini Ufaransa,Ujerumani na Uholanzi.
Mwanasiasa huyo kwa haraka amedai ushindi dhidi ya utawala aliopata Rais Donald Trump wa Marekani na kampeni ya kujitowa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya kuwa ni kukuwa kwa siasa za sera kali za mrengo wa kulia barani Ulaya.
Geet Wilders mwanasia mwenye ulimi mkali wa Uholanzi amelitumia jukwaa kurudia kauli yake dhidi ya Uislamu sera kuu ambazo zimekisogeza mbele chama chake cha uhuru (PVV) katika uchunguzi wa maoni kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo hapo mwezi wa Machi.
Amesema viongozi wa vyama vinavyotambulikana barani Ulaya wananadi sera yao kupinga kusilimishwa kwa bara hilo. wanasiasa huyo wa Uholanzi amesema hivi sasa wanawake wa Ulaya wanaogopa kuonyesha nywele zao za njano.
Afd yajiaandaa kuingia bungeni
Kiongozi wa chama Mbadala kwa Ujerumani AfD Frauke Petry ambaye chama chake kinajiandaa kuingia katika bunge la Ujerumani kwa mara ya kwanza mwaka huu ameishutumu Ujerumani na serikali za Umoja wa Ulaya kwa kutishia uhuru wa mtu binafsi na uhuru wa utamaduni kwa kupitia"upandikizaji wa mawazo" ambao amesema ni mbaya zaidi kuliko hata propaganda za kisoshalisti za mashariki.
Naye Matteo Salvini kiongozi wa chama sera kali za mrengo wa kulia cha Nothern League nchini Italia ametowa wito wa kujitowa katika kanda inaotumia sarafu ya euro ambayo amesema imeshindwa na ni jaribio la kihalifu.
Akitilia mkazo sera dhidi wahamiaji ambayo imekiwezesha chama chake kujiongezea umashuhuri katika miezi ya hivi karibuni kufikia kuungwa mkono kwa asilimia 15 nchini Italia Slavini amesema "Kuna maelfu ya Wataliana wasiokuwa na pa kukaa,hawana umeme au vipasha joto wakati maelfu ya wahamiaji wanaishi mahoteli."
Pia ameshambulia sera za wahamiaji za Merkel na kudai viongozi wa Ulaya wanauendeleza ugaidi kwa kuwapokea wakimbizi.
Takriban waandamanaji 3,000 wameandamana kupinga mkutano huo wakibeba mabango ya Hitler, Stalin na Mussolini na ujumbe wenye kosomeka "Ukiwa utalala kwenye demokrasia utaamka kwenye udikteta."
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/ dpa
Mhariri : John Juma