1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waanglikana waruhusu maaskofu wanawake

Charo, Josephat8 Julai 2008

Kanisa la kianglikana la England limepiga kura kuruhusu maaskofu wanawake licha ya kuwepo wasiwasi kwamba hatua hiyo huenda ikazusha mgawanyiko mkubwa.

https://p.dw.com/p/EYQA
Askofu mkuu wa kanisa la kianglikana Rowan WilliamsPicha: AP

Baraza kuu la kanisa la kiangalikana limepiga kura muhimu katika mkutano wake uliofanyika huko York kaskazini mwa England, kufuatia mjadala mkali kati ya viongozi wa kanisa hilo wasiotaka mageuzi na waliberali uliodumu muda wa saa nane. Kura hiyo ilipigwa na madaraja yote matatu ya kanisa hilo wakimewo maaskofu, makasisi na walei au washirika wa kawaida.

Maaskofu 28 walipiga kura kuunga mkono hoja ya kuchaguliwa maaskofu wa kike huku maaskofu 12 wakipinga hoja hiyo. Makasisi 124 waliunga mkono swala hilo lakini 44 wakapinga. Walei 111 walipiga kura kupitisha hoja hiyo huku 68 wakipinga.

Kanisa la kianglikana la England likiongozwa na askofu mkuu wa Canterbury Rowan Williams, ndilo kanisa lililoanzisha madhehebu ya kianglikana duniani yenye wafuasi takriban milioni 77. Kanisa hilo lliiwatawaza makasisi wa kike mnamo mwaka wa 1994 wakati kulipokuwa na mabishano makali kuhusu hatua hiyo.

Tofauti zajitokeza

Kwa viongozi wasiopendelea mageuzi katika kanisa la kianglikana, makasisi wa kike na wasenge, swala ambalo pia limezusha mipasuko ya kukwaza katika miaka michache iliyopita, yametilia shaka tafsiri ya kitabu kitakatifu cha dini ya kikristo, Biblia. Lakini viongozi wanaopendelea mageuzi katika kanisa hilo wanahoji wakati umewadia kuchukua mwelekeo wa kuwajumuisha wanawake.

Mchungaji mmoja aliyehudhuria mkutano huo wa sinodi, kasisi Ferial Etherington amenukuliwa na gazeti la The Times akisema, ``Inaonekena kama upuuzi mtupu kwangu kwamba kanisa linahubiri usawa kwa wote lakini wakati huo huo linaonekena likiwatenga baadhi ya watumishi wake waliowekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa kusema hawafai. ´´

Mkutano wa sinodi kuu hapo awali ulikataa hatua zilizonuiwa kuwajumuisha wale ambao hawangewakubali maaskofu wanawake. Pia mkutano huo ulipiga kura kupinga kuundwa kwa dayosisi mpya kwa parokia zinazopinga kuwepo kwa maaskofu wanawake.

Viongozi wenye ushawishi mkubwa katika kanisa la England, Rowan Williams na John Sentamu, askofu mkuu wa York, inaripotiwa walipendelea makubaliano yatakayozifurahisha pande zote mbili. Katika mahubiri yake ya Jumapili iliyopita Williams alisema Yesu alikuwa pamoja na wote waliokuwa katika pande zote mbili za mjadala huo. Lakini akasema angependelea kuwakubali wapinzani wa hoja ya kuwepo maaskofu wanawake kabla kikao cha jana kuanza.

Askofu mkuu wa York, John Sentamu mzaliwa wa Uganda amesema anayesafiri haraka, husafiri peke yake na anayesafiri kwenda mbali, husafiri pamoja na wengine. Yeye angependa kusafiri na kila mtu katika kanisa la kianglikana.

Watishia kulihama kanisa

Jumla ya makasisi 1,333 wametishia kulihama kanisa la kiangalikana ikiwa hawatapewa usalama wa kisheria kuunda mtandao wa parokia zitakazobakia chini ya utawala wa wanaume pekee. Wasiotaka mageuzi katika kanisa hilo sasa wanalazimika kuamua ikiwa wabakie kuwa washirika wa kanisa hilo au la, huku sherehe ya pamoja inayofanyika mara moja kila baada ya miaka kumi ikikaribia kufanywa wiki ijayo huko Canterbury kaskazini mwa England.

Padre David Houlding, kiongozi wa kanisa la kianglikana anayeshikilia desturi za kanisa hilo amesema hali ni mbaya na inaonekana kuna vuguvugu linalolishambulia kanisa kutoka kila upande na wanalazimishwa watoke.