1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wayalenga makazi ya kifalme Riyadh

Sylvia Mwehozi
19 Desemba 2017

Muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia unaopambana na waasi wa Kishia wa Yemen, umesema umezuia kombora lililorushwa kusini mwa Riyadh, wakati waasi wakisema waliyalenga makazi ya kifalme katika mji huo mkuu. 

https://p.dw.com/p/2peO0
Jemen Bürgerkrieg
Picha: Reuters/M. al-Sayaghi

Hii ni mara ya pili katika  kipindi cha miezi mingi ambapo kombora la waasi linafika mbali ndani ya makazi ya kifalme mjini Riyadh. Waasi wa Yemen wamesema kwamba wamerusha kombora hilo wakiyalenga makazi hayo ya kifalme ya Yamama mjini Riyadh, ambako Mfalme Salman hufanya mikutano ya kila wiki ya serikali na kupokea viongozi wakuu wa nchi mbalimbali.

Taarifa ya muungano wa jeshi iliyorushwa na televisheni ya taifa ya Saudi imesema kombora hilo lilirushwa na waasi wa Kihouthi, na kubainisha kwamba hakuna madhara yaliyotokea kutokana na kuzuiwa kwa kombora hilo. Wakazi wa Riyadh wamerusha video katika mitandao ya kijamii ikionyesha moshi kidogo angani baada ya kusikia mripuko mkubwa juu ya nyumba zao na wakati wakiendesha magari.

Jemen Bürgerkrieg
Wahouthi wakichukua hatua za kiusalama karibu na SanaaPicha: picture alliance/dpa/abaca/A. Homran

Nchini Yemen, msemaji wa kundi la Kihouthi Mohamed Abdul-Salam, amethibitisha kundi lake kurusha kombora hilo na katika ukurasa wake wa twitter aliandika kwamba walitumia kombora aina ya Volcano H-2.

Wakati hayo yakijiri, shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limesema jumla ya raia 136 wameuawa katika kipindi cha siku 10 na mashambulizi ya anga ya jeshi linaloongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen kwa mwezi huu.

Msemaji wa shirika hilo Rupert Colville amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa idadi ya watu walioujeruhiwa inafikia 87 katika mashambulizi hayo ya anga kati ya desemba 6 na 16. "Tuna wasiwasi na ongezeko la raia kujeruhiwa huko Yemen, kama matokeo ya mashambulizi makali ya anga yanayofanywa na muungano unaongozwa na Saudi, kufuatia kuuawa kwa rais wa zamani Ali Abdullah Saleh mjini Sanaa, siku ya Desemba 4," amesema Colville.

Schweiz Rupert Colville
Msemaji wa shirika la haki za binadamu la UN Rupert ColvillePicha: AFP/Getty Images

Mnamo Novemba 4, waasi hao waliulenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Riyadh na kikosi cha ulinzi cha anga cha Saudi Arabia kilisema kwamba shambulizi hilo liliweza kuzuiliwa, ingawa uchambuzi wa picha na video uliofanywa na gazeti la New York Times juu ya shambulio hilo ulionyesha kwamba kombora hilo liliharibika kwasababu ya kasi yake na nguvu.

Saudi Arabia ina mfumo wa Marekani wa kuzuia makombora ya ardhini na angani, ambao rais Donald Trump aliusifu kwa kufanikiwa kuzuia kombora la Novemba 4. Katika muda wa karibu miaka mitatu ambayo muungano wa jeshi unaongozwa na Saudi Arabia umepambana na waasi wa Yemen, makombora kadhaa yameruhushwa na waasi hao wa Kihouthi katika mipaka ya Saudi Arabia, na kufikia mbali hadi kwenye mipaka ya mjini. Mapema mwezi huu waasi hao walidai kwamba walirusha kombora katika kinu cha nyuklia kilichoko katika matengenezo katika nchi ya Falme za Kiarabu ambayo ni sehemu ya muungano wa jeshi unaongozwa na Saudi Arabia linalopambana na makundi ya wanamgambo wa Yemen.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga