Wabunge Korea Kusini wamuondoa Han Duck Soo madarakani
27 Desemba 2024Idadi ya wabunge 192 ya bunge linalodhibitiwa na upinzani, walipiga kura ya kumuondoa Han madarakani. Chama tawala cha People Power kilisusia kupiga kura na kukusanyika karibu na alipokaa spika wa bunge Woo Won Shik, huku wakisema kwa sauti kuwa kura hiyo ni batili na wakimtaka Woo ajiuzulu.
Wabunge wa chama hicho waliandamana baada ya Woo kuitisha kura ya kuondolewa kwa Han Duck Soo, akisema kupita kwa kura hiyo kutahitaji wingi wa kura katika bunge hilo lililo na wanachama 300 na sio theluthi mbili ambayo chama cha PPP ilidai inahitajika ili kumuondoa Han.
Upinzani Korea Kusini waanzisha mchakato wa kumg'oa Kaimu Rais
Baada ya kura hiyo kupita na Han kukabidhiwa nyaraka za kuondolewa kwake na mahakama ya katiba, waziri wa fedha na naibu waziri mkuu Choi Sang Mok anatarajiwa kuchukua nafasi ya Han kama kaimu rais wa Korea Kusini. Han alichukua nafasi hiyo baada ya rais Suk Yeol kuondolewa na bunge la taifa tarehe 14 Desemba baada ya kutangaza amri ya kijeshi.
Chama kikuu cha upinzani cha Democratic kimemtuhumu Han kushirikiana na Yoon katika uamuzi wake wa kutangaza amri hiyo na pia kama kaimu kiongozi, anazuia uchunguzi dhidi ya Yoon na kuzuwia pia kukamilika mchakato wa kumuondoa Yoon madarakani. Mahakama ya katiba Korea Kusini ilianzisha kesi ya kumuondoa Yoon mapema siku ya Ijumaa iliyopita, na katika wiki chache zijazo mahakama itaamua iwapo kura ya kumuondoa Yoon iliyopigwa bungeni, iliendana na matakwa ya katiba ya nchi hiyo.
Mahakama ya katiba kuamua hatma ya Yoon
Majaji wakihakiki kuondolewa kwa Yoon, Uchaguzi mpya utapaswa kuandaliwa ndani ya siku tisini baada ya hatua hiyo kutangazwa. Lakini wakibatilisha uamuzi wa bunge basi Yoon atakuwa huru kurejea tena madarakani. Angalau majaji sita wanapaswa kuhakiki uhalali wa kura hiyo ya kumuondoa Yoon madarakani maana ni majaji hao sita tu walio na nafasi ya kufanya hivyo kati ya nafasi 9 zilizopo katika mahakama hiyo ya katiba.
Rais Yoon wa Korea ashindwa kufika kwa mahojiano ya ufisadi
Na kura moja tu ya kupinga kura ya bunge, inaweza kufanya mchakato mzima wa kumuondoa Yoon kwenda kombo. Hatua hiyo huenda ikaididimiza nchi hiyo katika mzozo mkubwa zaidi wa kisiasa, kuathiri uchumi na kuiharibia sifa kimataifa. Moja ya matakwa ya wabunge wa upinzani kwa Han ilikuwa kuwateua majaji wengine watatu kuongeza idadi ya majaji kuwa tisa katika mahakama hiyo jambo ambalo Han hakuliridhia.
Uamuzi wa Yoon wa kutangaza amri ya kijeshi uliishutua Korea Kusini pamoja na washirika wake lakini ulipingwa saa chache baadae kufuatia maandamano makubwa dhidi yake. Aliwataja wapinzani wake kama kikosi hatari kwa taifa na kutetea uamuzi wake akisema ni wakuilinda Korea Kusini.
ap, dpa