Wabunge wanawake Rwanda wavunja Rekodi
22 Oktoba 2003
Rwanda imeweka rekodi ikiwa ndiyo nchi yenye idadi kubwa ya wanawake bungeni duniani, kufuatia uchaguzi wa mwezi huu. Taarifa ya Umoja huo wa wabunge Ulimwenguni mjini Geneva imesema kwamba taifa hilo dogo la Afrika kati-Rwanda sasa limechupa na kushika nafasi ya kwanza kutoka ile ya 23 na kuwa na wabunge wengi kabisa wanawake Ulimwenguni , ikiipiga kumbo Sweden ambayo hadi sasa ndiyo iliokua ikishikilia nafasi hiyo.
Wanawake sasa wanauakilishi wa 48.8 asili pia katika bunge la taifa nchini Rwanda baada ya matokeo ya uchaguzi wa mapema mwezi huu, ukiwa ni wa kwanza tokea mauaji ya halaiki ya 1994 ambapo karibu Watutsi na wahutu wa msimamo wa wastani jumla ya milioni moja waliuwawa. Ama uakilishi wa wanawake katika bunge la Sweden ni 45 asili mia.
Katibu mkuu wa Umoja wa wabunge duniani Anders Johnsson alisema wanaamini matukio hayo ni mafanikio kwa taifa hilo kwa jumla, kwani wanawake hutoa mchango maalum katika kazi za bunge, wakiwa na mtazamo tafauti na ule wa wanaume panapohusika na masuala ya jamii. Bw Johnsson akaupongeza uchaguzi wa Rais na Bunge nchini Rwanda licha ya dosari zilizotajwa na Umoja wa Ulaya, akiisitiza kwamba ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imetoka katika janga kubwa la mauaji miaka 10 iliopita, hii inaweza kuwa ni hatua moja mbele baada ya baada ya kupitia njia ndefu na ngumu. Alisema wanawake nchini Rwanda wamepigana muda mrefu hadi kufikia hapa. Katika uchaguzi wa Rais Kiongozi wa muda mrefu sasa Paul Kagame ndiye aliyetangazwa mshindi kwa kujinyakulia takriban 95 asili mia ya kura na katika uchaguzi wa bunge chama chake Rwandan Patriotic Front kikashinda kwa wingi mkubwa bungeni, ambamo chini ya katiba mpya wanawake tayari wanahakikishiwa viti 24. Sambamba na viti hivyo wanawake wakashinda viti 15 zaidi vilivyogombewa pamoja na kuwa na vyengine 6 katika Baraza la Senate.
Hivi sasa suali linaloulizwa ni jinsi gani uakilishi mkubwa wa wanawake utakavyoweza kuleta maendeleo katika siasa za Rwanda. Miongoni mwa changa moto zinazowakabili akina mama nchini Rwanda bila shaka ni pamoja na kupambana na mtindo wa ndoa kwa njia ya ubakaji, jambo ambalo limekua likizitia asi wasi mno jumuiya za wanawake nchini humo. Mtindo huo wa kusaka mke kwa kumbaka msichana unayetaka kumuowa unatajwa kuwa unatokana na taratibu za kijadi, lakini makundi ya kupigania haki za binaadamu yanazieleza kuwa zilizopitwa na wakati na pia ni ukiukaji wa haki ya mwanamke. Kwa kawaida wahanga wakubwa zaidi ni ni wasichana kati ya miaka 16 na 22.
Mafanikio ya wanawake katika siasa katika nchi za Nordic yaani Sweden, Denmark, Norway na Finland kwa mfano kwa muda mrefu yametajwa kua ni yenye kutokana na utamaduni ambao kimsingi huthamini usawa na mchango wa wanawake katika sekta zote za jamii. Kwa hivyo wakati ndiyo utakaotambulisha iwapo nchini Rwanda nako utamaduni utaweza kutoa mchango kama huo au la. Kwa mujibu wa tarakimu, kiwango cha uakilishi wa wanawake katika siasa kwa mtazamo jumla duniani ni 15.2 asili mia- na wa Umoja wa wabunge duniani unasema hicho ni kiwango cha juu kuwahi kufikiwa hadi sasa.