1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachina 17 wakamatwa Kongo kwa kuendesha mgodi haramu

21 Desemba 2024

Wanaume 17 raia wa China wamekamatwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa tuhuma za kuendesha shughuli za uchimbaji madini katika mgodi haramu wa dhahabu.

https://p.dw.com/p/4oSHF
Dhahabu ya Kongo
Uchimbaji haramu wa dhahabu ni changamoto kubwa kwa serikali mjini Kinshasa.Picha: Mariel Müller/DW

Hayo yameelezwa na mamlaka za nchi hiyo wakati serikali ikiendelea kukabiliana na vitendo vya uchimbaji wa madini bila vibali. Kwa sasa, wachina hao wanashikiliwa katika mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kusini wa Bukavu.

Waziri wa fedha wa jimbo hilo na kaimu waziri wa madini Bernard Muhindo amesema watu hao walikamatwa baada ya ujumbe wa serikali kufanya ukaguzi wa kushtukiza walipotembelea eneo la mgodi katika kijiji cha Karhembo siku ya Alhamisi.

Waziri Muhindo ameongeza kuwa takriban raia 60 wa China na wengine kadhaa wakiwa ni raia wa Kongo na Burundi walikuwa mgodini hapo, lakini maafisa waliamua kuwaweka kizuizini watu 17 walioonekana kuwa wasimamizi.