1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wazungumzia siku ya wanawake duniani

Abdu Said Mtullya8 Machi 2011

Akina mama washerehekea miaka mia moja ya harakati zao za kupigania haki

https://p.dw.com/p/10VWd
Maadhimisho ya mwaka wa mia moja wa siku ya wanawake duniani.Picha: UN Photo/Ky Chung

Magazeti Ujerumani leo yanatoa maoni juu ya mwaka wa mia moja wa siku ya wanawake duniani kwa kuiangalia Ujerumani.

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linawata akina baba wauthamini mchango unaotolewa na wanawake katika maendeleo ya jamii. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba wanawake ndiyo,wazazi, ndiyo akina mama wa majumbani na pia ni wafanyakazi. Mambo hayo matatu yanashikamana ,anasema mhariri wa Stuttgarter Nachrichten. Kwa hiyo kila siku ingelikuwa siku ya wanawake duniani, laiti pangekuwa na mtazamo sahihi wa kijamii.

Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anazungumzia juu ya ubaguzi unaowakabili wanawake ,hata baada ya miaka 100 tokea waanze kupigania haki zao.Mhariri huyo anasema ingawa akina dada aghalabu wanawaacha nyuma akina kaka inapohusu ufanisi wa shuleni, sehemu za uongozi kwenye makampuni na viwandani nchini Ujerumani bado ni hodhi ya wanaume . Kwa hiyo Kansela Merkel ana haki ya kusema kwamba Ujerumani bado ipo nyuma,katika vipimo vya dunia, inapohusu nafasi za uongozi kwa wanawake nchini. Lakini Kansela huyo ajue kwamba kauli tupu hazitasaidia.Kinachotakiwa ni hatua za kuishinikiza jamii.

Mhariri wa gazeti la Mindener Tageblatt anakumbusha juu ya mafanikio yaliyofikiwa na wanawake katika miaka mia moja iliyopita. Lakini anasema, ili kuleta usawa, haitoshi kuzungumzia juu ya jinsia tu. Mhariri huyo anafafanua kwa kusema haki ya kupiga kura kwa akina mama, haki ya kuchagua kazi ya kufanya pamoja na haki ya kupatiwa huduma za afya:- mafanikio hayo yamepiganiwa na bibi na mama zetu ,barabarani na mabungeni. Jambo muhimu katika mabadiliko, siyo hatua ya kwanza, bali ukakamavu wa kuyaendeleza mabadiliko hayo. Lazima tujifunze hayo, kwani katika suala la kuleta haki sawa, kinachohitajika ni zaidi ya utambulisho wa jinsia. Nasaba ya mtu,elimu, na hata mahala ambapo mtu amezaliwa ni miongoni mwa mambo muhimu katika kuleta usawa kwa wanawake.

Katika maoni yake gazeti la Heilbronner Stimme linasisitiza umuhimu wa malezi ya watoto.Gazeti hilo linasema katika kuadhimisha mwaka wa mia moja wa siku ya wanawake duniani, litakuwa jambo la manufaa ikiwa Ujerumani itaweka utaratibu wa kazi utakaowafiki na mazingira yanayowakabili wanawake.

Utaratibu huo maana yake ni kuoanisha kazi za akina mama na ulezi wa watoto wao kwa kujenga vituo kwa ajili ya malezi ya watoto.Na watakaonufaika na utaratibu huo, hawatakuwa wanawake tu.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten anatoa mfano wa hadhithi ya punda, baba na mtoto kuhusiana na wanawake.Wale wasiokuwa na watoto, wanaitwa makatili, wale wanaoamua kukaa nyumbanina kulea watoto, wanachekwa, na wale wanaoyachanganya yote, wanaitwa wabinafsi.Mhariri anasema laiti jamii ingeliikabili hali hiyo,hiyo ingelikuwa hatua kubwa sana.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Othman Miraj