1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wadai nafasi zaidi za wanawake katika maamuzi Kenya

Mohamed Dahman24 Februari 2007

Wanaharakati nchini Kenya wako mbioni kudai mageuzi ya katiba yatakayohakikisha kwamba wanawake zaidi wanapatiwa nyadhifa za kupitisha maamuzi katika serikali badada ya kuwa tu washangiliaji,waimbaji na wacheza ngoma kwa ajili ya wagombea.

https://p.dw.com/p/CBHS
´Wanawake wakiandamana nchini Kenya hivi karibuni kudai haki za wanawake wakati wa Kongamano la Kijamii Duniani
´Wanawake wakiandamana nchini Kenya hivi karibuni kudai haki za wanawake wakati wa Kongamano la Kijamii DunianiPicha: AP

Harakati hizo zinapamba moto wakati nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikitarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu mwezi wa Desemba mwaka huu.

Kuna wabunge 18 wanawake kati ya wabunge 222 nchini Kenya.Wakati hii ni idadi kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo bado ingali ni pungufu ya asilimia 10 kwa ujumla.

Kundi jipya la Muungano wa Katiba linaamini kwamba idadi ya viti bungeni ambapo kwayo wabunge huteuliwa badala ya kuchaguliwa inapaswa kuongezwa kutoka 12 hadi 36 ambapo 24 vitengwe kwa ajili ya wanawake.Hilo ni mojawapo ya maombi 12 ya mageuzi ya katiba ambayo kundi hilo linataka yatekelezwe kabla ya uchaguzi.

Hata hivyo baadhi wanasema kwamba ombi la kundi hilo sio la kutosheleza katika kuhakikisha kwamba Kenya ina asilimia 30 ya nyadhifa muhimu za serikali zinazoshikiliwa na wanawake. Kuhusiana na bunge kiwango cha asilimia hiyo 30 ya viti kinaonekana na wengi kuwa kiwango cha chini ambacho kinahitajika ili sauti za wanawake ziwe na uzito bungeni.

Lakini Njoki Ndung’u mjumbe wa kamati ya bunge juu ya Utawala wa Masuala ya Sheria na Haki anasema mageuzi hayo yatakuwa hatua ya maana ya kuanzia kuelekea usawa wa jinsia. Amesema hiyo ni idadi ya wale walioteuliwa tu na kwamba ukiongeza na wale wa kuchaguliwa idadi itakuwa kubwa zaidi kuliko ile iliopo hivi sasa.

Mjadala juu ya muswada huo unatazamiwa kuanza wakati bunge litakapokutana mwezi ujao. Majaribio ya huko nyuma ya kushinikiza sera za hatua za vitendo kushajiisha uwakilishi wa wanawake yamekwenda kombo.

Hatua za kujashiisha usawa wa kijinsia na uwakilishi wa wanawake tayari zimepata mshiko katika nchi jirani na Kenya. Uganda imeongeza uwakilishi wa wanawake bungeni kufikia asilimia 24 wakati nchini Tanzania umefikia asilimia 15 kwa kutumia vifungu vya katiba kutekeleza hatua hizo.

Rwanda ndio imetia fora kwa hilo ambapo ina wanawake takriban asilimia 49 katika nyadhifa za bunge.

Kwa mujibu wa Irene Oloo mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wapiga Kura Wanawake nchini Kenya hatua za kushaajisha uwakilishi wa wanawake kwa matamko ya katiba ni njia moja tu ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika siasa uwanja ambao huko nyuma ulikuwa umetengwa kwa wanaume tu.

Lakina aidha kwa kuwapo shajiisho hilo kikatiba au la wanawake nchini Kenya bado wanaweza kukabiliwa na kejeli, vitisho na kushambuliwa kimwili kama yalivyomkuta Monica Amolo wakati akijaribu kugombania kiti cha ubunge magharibi mwa Kenya hapo mwaka 2002.Mama huyo ilibidi avumulie matusi na maonevu kutoka kwa mpinzani wake wa kiume ambaye alikuwa akimwita kila aina ya majina kuanzia kahaba hadi mvunja ndoa.

Shirika moja linalojishughulisha na masuala ya habari na maendeleo linalojulikana kama African Women and Child lenye makao yake mjini Nairobi linasema katika mazingira ya uchaguzi kama hayo wanawake wanaoshiriki kwenye kampeni takriban hufanywa kuwa washangiliaji tu,waimbaji na wacheza ngoma kwa ajili ya wagombea.

Muswada wa vyama vya kisiasa tayari umewasilishwa bungeni ukitaka kufutwa kwa vyama vya kisiasa na kuzuiliwa kwa wagombea wanaojihusisha na maonevu,vurugu,hotuba za chuki na uchochezi.