1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wanajikuta mikononi mwa wanamgambo

13 Julai 2015

Wanamgambo wenye misimamo mikali wamekuwa wajuzi wa kutumia mtandao wa intaneti kueneza propaganda kuwavutia wanawake wa Ujerumani. Kupitia mtandao huu Dola la Kiislamu huwavutia wapiganaji, wake na akina mama wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1FxkW
Deutschland Verschleierte Frau Nigab (Symbolbild)
Picha: picture-alliance/dpa/P. Endig

Wasichana wadogo wanaendelea kukimbia kutoka kwao na kuwaacha wazazi wao wenye huzuni Ujerumani kwenda kujiunga na kundi la Dola la Kiislamu IS nchini Syria na Iraq. Kundi hilo tayari limeyadhibiti maeneo makubwa ya nchi hizo mbili, yakidai ni himaya yao ya utawala wao mpya ambapo wanamgambo hao hutumia Sharia za kiislamu.

Propaganda ya IS inayowalenga wanawake haitumii majukwaa makubwa kwa mujibu wa Florian Endres, mtaalamu wa itikadi kali katika Ofisi ya Uhamiaji na Wakimbizi ya Ujerumani, BAMF.

"Wanatumia makundi na majukwaa madogo ambako wanaweza kuwafikia wasichana na wanawake wa mataifa ya magharibi, kujaribu kuwashawishi kuwa sehemu ya jamii hii ya Dola mpya ya Kiislamu," amesema Endres wakati alipozungumza na DW na kuongeza kuwa kundi la Dola la Kiislamu linaunda taifa jipya na kwa kufanya hivyo linahitaji wanawake kuanzisha familia.

Kuwashawishi akina dada wa Ulaya

Endres amesema wasichana ambao tayari ni sehemu ya jamii ya Salafi nchini Ujerumani wanaitumia sana mitandao ya kijamii, ambamo hueneza taarifa. Ameongeza kuwa mawasiliano yanafanyika kwa pande zote mbili - mara nyingine mtu anatafuta taarifa kuhusu vipi anavyoweza kwenda Syria au Iraq na mara nyingine wasichana wanafuatwa na wanawake ambao tayari wamesafiri na kujiunga na IS. "Wanaripoti moja kwa moja wakiwa huko kuhusu vipi maisha yalivyo mazuri huko," amesema Enders.

Screenshot Twitter Muhajira
"Nilihama kwa ajili ya Allah," anasema mwanablogu huyo

Mwanamke Mjerumani anayejiita "Muhajira", jina linalomaanisha mhamiaji, amekuwa akiandika taarifa katika blogu na kutuma katika mtandao wa facebook na Twitter tangu alipoondoka Ujerumani mnamo mwaka 2013. Ameandika kuhusu maisha yake nchini Iraq na msingi wa vita vitakatifu vya Jihad na msingi wa heshima. Katika ripoti yake ya hivi karibuni aliyoituma "Muhajira" amesifu jinsi hatimaye alivyo huru kuvaa niqab atakavyo bila kuona wala kusikia dhihaka baada ya kuondoka Ujerumani.

Mwanablogu huyo anatoa maelezo na ahadi ya taarifa zozote ambazo wanaotaka kuwa wake wa wapiganaji wa Jihadi huenda wakazihitaji. Pia yuko tayari kutafuta wasichana kwa ajili ya wapiganaji hao "kwa sababu kuna wasichana wengi mujahedeen ambao bado hawajaolewa hapa Ujerumani."

Kuyatukuza maisha katika Dola ya Kiislamu

Kuna taarifa nyingi katika Twitter na blogu zinazoonekana kuandikwa na wanawake wa mataifa ya Magharibi walioolewa na wanamgambo wanaopigana katika kundi la Dola la Kiislamu na kujenga jamii mpya ya waislamu. Wasichana hao wadogo husifu kuhusu fahari ya maisha ya familia na kulea watoto kuwa wapiganaji wapya wa kuutetea Uislamu.

Barani Ulaya wasichana hugeukia Twitter na tovuti ya ask.fm, jukwaa la maswali na majibu kuhusu vipi kusafiri kwenda Syria au Iraq. Suala linaloulizwa mara kwa mara ni vipi kuwashughulikia wazazi waliokata tamaa wanaokataa kuwaruhusu wasichana wao kuondoka nyumbani kwenda kujiunga na vita vya Jihad. Kupata ruhusa ya mzazi kunaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 wanaohitaji idhini ya mzazi kuweza kusafiri au kuoelewa.

Endres anasema Ofisi ya Uhamiaji na Wakimbizi ya Ujerumani, BAMF, hujaribu kuwasaidia wazazi kuwazuia wasichana wao kushawishiwa kuwa na misimamo mikali ya kidini na kuondoka nyumbani, lakini ni kibarua kigumu sana. Endres aidha amesema wasichana hao wadogo hawafahamu lolote kuhusu siasa na dini, kitu kinachowafanya kuwa rahisi kushawishika.

Kwa mujibu wa Idara ya Ujasusi ya Ujerumani, takriban asilimia 40 ya wasichana na wanawake wanaokadiriwa kuondoka Ujerumani kujiunga na makundi yenye misimamo mikali ya kidini, wana umri wa chini ya miaka 25 na baadhi yao wangali chini ya umri wa miaka 18. Wanaume wapatao 650 waislamu wa Ujerumani na zaidi ya wasichana 100 wamefaulu kujiunga na makundi ya wanamgambo nchini Syria na Iraq.

Mwandishi:Josephat Charo/dw.com/english

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman