Wanasiasa wa Ufaransa wanakutana kujadili serikali mpya
10 Desemba 2024Mkutano huu unajiri siku chache tu baada ya Waziri Mkuu Michel Barnier kuondolewa kupitia kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye. Huku wakivifungia nje vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia, National Rally - RN, na mrengo mkali wa kushoto, France Unbowed - LFI, wanasiasa wanatafuta njia ya kusonga mbele, wakati mawaziri wa muda wakihangaika kuiweka sawa bajeti ya Ufaransa kwa mwaka wa 2025, baada ya serikali ya awali kushindwa katika mipango yake ya kupunguza gharama ya bajeti.
Rais Macron alisema jana usiku kuwa lengo ni kusonga mbele na makubaliano kuhusu mbinu itakayotumika ya kuunda serikali mpya katika misingi isiyo imara ya bunge ambalo halina chama chenye wingi wa viti. Haijulikani ni jinsi gani viongozi wanaweza kujenga msingi mpana wa uungwaji mkono kwa serikali yoyote mpya.