Wanawake hawajawezeshwa kujiepusha na ngono
16 Mei 2006Vilabu vya True Love Waits katika shule za mjini Kampala na miji mingine ya Uganda vilianzishwa na shirika liliso la kiserikali la Family Life Network, mtandao wa maisha ya jamii. Shirika hili lina lengo la kuinua kiwango cha tabia njema katika maisha ya jamii kupitia familia. Wanaokula kiapo cha uanachama hupewa kadi zinazoonyesha kwamba wao sasa wameamua kujiepusha mbali na ngono.
Mkurugenzi mtendaji Stephen Langa anasema wanafunzi takriban elfu 13 walio na umri kati ya miaka 13 na 20 wamejiunga na vilabu hivyo mjini Kampala pekee. Uganda ilikuwa nchi mojawapo duniani ambako ukimwi uliwaua watu wengi katika miaka ya 1980 na 1990. Lakini hali hii ilibadilika wakati nchi hiyo ilipoanzisha sera ya ABC dhidi ya ukimwi, yaani kujiepusha na ngono, kuwa mwaminifu au kutumia kondomu.
Kwa wakati huu idadi ya maambukizi ya ukimwi nchini Uganda yamepungua kufikia asilimia tano ikilinganishwa na asilimia 20 katika miaka ya 1990. Wataalamu wanasema haya ni matokeo ya hatua ya serikali kuunga mkono kwa dhati ngono kutumia vizuizi kwa kuanzisha sera ya matumizi ya kondomu. Hata hivyo mkakati huu ulibadilika mwaka jana kwa kuhimiza watu wajiepushe na ngono, huku matumizi ya kondomu yakielekezwa kwa maeneo yalioathiriwa sana na ukimwi.
Mratibu wa mtandao wa wanawake wa Uganda, UWONET, Salome Nakaweesi Kimbugwe hafikiri mpango wa kujiepusha na ngono unazingatia ukweli wa mambo nchini Uganda. Wanawake wa Uganda wamo mikononi mwa wanaume linapokuja swala la ngono, amesema Bi Kimbugwe. Itawezekana vipi mwanamke kujizuia kufanya ngono ikiwa yeye mwenyewe hana uwezo juu ya mwili wake? Hawezi kuamua ni lini, wapi, vipi au na nani anataka kufanya ngono.
Katika mahojiano yake na shirika la habari la IPS Kimbugwe alisema wanawake wa Uganda hawajawezeshwa kufanya uamuzi juu ya ngono na kuweza kumwambia mwanamume sitaki. Wanawake hawaruhusiwi kuzunguzia wazi swala la ngono.
Utamaduni pia unachangia kuendeleza hali hii. Katika maeneo ya kati na mashariki mwa Uganda, ni jukumu la makungwi wanaowafunza wasichana waliovunja ungo kuhusu ujuzi katika maswala ya ngono kuwahimiza wasichana hao kuwa tayari kufanya ngono na waume zao kila wakati.
Ida Nakabungo, ni mama wa watoto watatu na mkaazi wa kitongoji cha Mengo mjini Kampala. Anasema hawezi kumkatalia mumewe ngono kwa hofu ya kupigwa na kufukuzwa nyumbani. Anaamini pia kwamba wanaume wote hudanganya katika ndoa na kuwaweka wake zao katika hatari ya kuambukizwa ukimwi.
Usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake ni lengo la tatu katika orodha ya malengo ya maendeleo ya Milenia. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya shirika la umoja wa mataifa la mpango wa maendeleo, UNDP, wanawake hawana nafasi nzuri katika jamii kwa sababu ya kazi za nyumbani, ndoa za mapema na kubeba mimba.
Umaskini, utamaduni na dini vinawalazimu wazazi wa Uganda kuwaoza mabinti zao wakiwa bado chini ya umri wa miaka 18. Itawezekana vipi kuzuia kuenea kwa ukimwi ikiwa hali ni hii? Ndio maana watetezi wameitaka serikali ya Uganda kuipitisha misuada ya mahusiano ya kijamii na makosa ya kijinsia bungeni. Msuada wa kwanza unashughulikia swala la mahari, kuoa zaidi ya mwanamke mmoja, mwanamke na mwanamume kuishi pamoja, ubakaji katika ndoa na ukeketaji.