Wanawake wa Kisaudi wapinga marufuku ya kuendesha gari
17 Juni 2011Wito huo wa kuandamana kupinga utamaduni unaopiga marufuku wanawake kuendesha magari nchini Saudi Arabia, ulitumwa kwenye mtandao wa kijamii wa facebook na twitter na kuvutia wanawake wengi.
Maandamano haya yameelezwa kuwa makubwa, ikilinganishwa na ya mwaka 1990, ambapo kundi la wanawake 47 walikamatwa na kuadhibiwa vikali baada ya kuandamana wakiendesha magari kupinga tamaduni hiyo.
Tawfiq Alsaif, mwandishi wa makala maalumu, amesema kwenye twitter kuwa mke wake aliamua kuanza siku ya leo kwa kuendesha gari kwenda supamarket na kurudi nyumbani.
Maha al Qahtani amesema kwenye twitter kuwa aliamua gari kwa siku ya leo iwe yake na kuendesha kupitia barabara ya King Fahd na mtaa wa Olaya, akiwa na mume wake ndani ya gari.
Mohammed al-Qahtani amesema mke wake alichukuwa bidhaa zake muhimu, tayari kwenda jela bila woga wowote kama angekamatwa na polisi.
Mwanamke mmoja aliyetuma video yake kwenye mtandao akiwa ndani ya gari, amesema anaamini jamii iko tayari kuwa na wanawake wanaodesha magari na wanachotaka ni kuweza kufanya shughuli zao bila kutegemea madereva.
Mwanaharakati mmoja anayejiita Hayat amesema, "Hili si suala la kampeni ya tarehe 17 June, lakini ni kampeni ambayo ni kubwa zaidi ya hapo. Inarudi kwenye harakati za miak 20 nyuma. Mwezi wa Juni ni alama tu ya mapambano ya kutafuta haki ya mwanamke nchini Saudi Arabia. Hi ni Sawa na harakati za haki za kiraia kama vile wanaume wanavyopigania haki zao"
Mwanaharakati wa masuala ya wanawake, Wajiha al Huwaidar, amesema hatazamii kitu kikubwa kama nchi za magharibi zinavyotarajia kutokana na hatua kali zilizochukuliwa dhidi ya wanawake ambao walishawahi kujaribu kufanya hivyo.
Al Huwaida amesema kufungwa kwa Manal Al-Sharif, mtaalamu wa sayansi ya komputa, mwenye miaka 32 na wengine waliojaribu kupinga tamaduni hiyo, kumewatia hofu wanawake wengi nchini humo.
Kwa mujibu wa mpiga picha wa shirika la habari la Ufaranza, AFP, usalama katika mji wa Riyadha ulikuwa wa kawaida.
Hayati anasema, "Katika kila jamii kuna kuwa na upinzani dhidi ya mageuzi, hata katika nchi za magharibi kulikuwa na upinzani mkubwa wakati walitaka kujikomboa kutoka katika utumwa. Na wengine wamepambana sana katika kujiondoa kwenye utumwa."
Ujumbe wa kampeni hiyo kwenye mtandao wa kijamii wa facebook umesema zoezi hilo litaendelea hadi mfalme atoe agizo linaloruhusu wanawake kuendesha magari.
Amnesty Internationa imesema jana kuwa polisi nchini Saudi Arabia lazima ziache kuwachukulia wanawake kama raia wadaraja la pili, na kuruhusu wanawake kuendesha magari.
Hakuna sheria inayopiga marufuku wanawake kuendesha magari katika nchi hiyo yenye utajri wa mafuti, lakini wizara ya mambo ya ndani imeweka kanuni kwa mujibu wa fatwa zinazosema wanawake wasiruhusiwe kuendesha magari.
Mwandishi: Rose Athumani/AFP/DPA
Mhariri: Miraji Othman