1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wahimizwa kuendeleza harakati za kutetea haki zao

8 Machi 2006

Viongozi kutoka nchi mbali mbali waadhimisha siku ya wanawake duniani na kutoa miito kuwataka wanawake waendeleze harakati za kupambana na ubaguzi dhidi yao.

https://p.dw.com/p/CHnf
Kansela wa Ujerumani bibi Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani bibi Angela MerkelPicha: AP

Katika risala yake ya kuiadhimisha siku ya wanawake duniani bibi Angela Merkel mwanamke wa kwanza kuwa kansela wa Ujerumani amesema kwamba wanawake wanapaswa kuikumbuka siku hii kama siku inayowataka waendeleze harakati za kutetea haki ya usawa wa kijinsia.

Kansela Merkel amesema, siku hii ni ya muhimu sana kwani inakumbusha yale yaliyoafikiwa na wanawake katika sehemu mbali mbali ulimwenguni.

Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia rais wa kwanza mwanamke barani Afrika alikuwa mgeni wa heshima huko Paris Ufaransa katika sherehe za siku ya wanawake duniani.

Awali rais Jacque Chirac wa Ufaransa alisema kuwa bibi Ellen Johnson Sirleaf ni mfano bora wa jinsi wanawake wanavyo changia katika maendeleo ya bara la Afrika.

Bibi Sirleaf katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani alihudhuria mkutano juu ya maendeleo na tafrija kadhaa za shirika la elimu na utamaduni la umoja wa mataifa UNESCO na baadae kuhudhuria dhifa ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa kwa heshima yake. Tafrija hiyo pia ilihudhuriwa na bibi Shirin Ebadi mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kutoka Iran.

Rais Carlo Azeglio Ciampi wa Italia katika risala yake ya siku hii ya wanawake duniani, amewataka wanaume kutoa mchango zaidi katika malezi ya watoto ili kuwapunguzia mzigo mzito wa kazi ya ulezi wanawake ambao wana haki sawa na wanaume.

Kwa miaka kadhaa umoja wa mataifa umekuwa unazingatia kuleta maendeleo ya wanawake katika nyanja nne zikiwa ni katika maswala ya sheria, kushirikishwa wanawake katika maswala ya kimataifa, mafunzo na utafiti unaohusisha takwimu juu ya mambo ya jinsia pamoja na misaada kwa wanawake wenye hali duni.

Mwito wa mwaka huu wa 2006 ni Wanawake kushiriki katika kupitisha maamuzi, lengo la umoja wa mataifa katika kutekeleza mwito huo ni kuhakikisha kuwa wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika kutatua matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Nchini Malaysia binti wa aliyekuwa waziri mkuu Mahathir Mohamad ameifananisha hali ya wanawake wa kiislamu nchini humo na hali iliyowakabili wanawake wa kiafrika wakati wa siasa ya ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini.

Bi Marina Mahathir mwanaharakati wa haki za wanawake na muandishi wa makala ya jumatano katika gazeti la The Star nchini Malaysia amehoji ubaguzi unaowakabili wanawake wa kiisalmu nchini humo.

Katika kuisherehekea siku hii kamati yakimataifa ya olimpiki huko mjini Geneva imemtunukia tuzo la mwanaspoti bora mwanamke wa mwaka 2006, aliyekuwa kinara wa mchezo wa tennis wa Argentina bibi Gabriela Sabatini kwa juhudi zake za kuuboresha mchezo huo. Tuzo kama hiyo imetunukiwa wanawake wengine watano ulimwenguni. Akiwemo bibi Albertine Barbosa Andrade kutoka Senegal.