1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WANAWAKE WATATHMINI SERA YA BEIJING

Mohamed Dahman28 Februari 2005

Maelfu ya viongozi wa kike kutoka duniani kote wanakutana wiki hii kwa ajili ya tathmini kuu ya kimataifa juu ya kile ilichokifanya Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 10 iliopita kuhakikisha haki sawa kwa wanawake katika nyanja zote za maisha. Ujumbe wao kwa Umoja wa Mataifa kwamba sasa hakuna visingizio tena wala kucheleweshwa tena.

https://p.dw.com/p/CHhM
WANAWAKE WA BANGLADESH WAKIHANGAIKA NA MAISHA
WANAWAKE WA BANGLADESH WAKIHANGAIKA NA MAISHAPicha: dw

Wajumbe kwenye mkutano wa nne wa Viongozi Duniani katika mji mkuu wa China Beijing hapo mwaka 1995 wametowa ahadi maalum kutenguwa sheria zote zinazowabaguwa wanawake na kupitisha sera ambazo zitastawisha usawa wa jinsia katika maisha ya watu.

Je ni kwa kiasi gani wamefanikiwa kutsafsiri kwa vitendo ahadi zao hizo?

Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa na mashirika makuu yasio ya kiserikali hawakufanikiwa vya kutosha!

Kyung-wha Kang anayeongoza tume ya Umoja wa Mataifa juu ya Hadhi ya Wanawake yenye wajumbe 45 anasema hawakuridhika na kuna mengi yanayohitajika kufanywa.

Carolyn Hannan afisa mwandamizi katika Idara ya Uchumi na Masuala ya Kijamii ya Umoja wa Mataifa anakubali kwamba maendeleo yamepatikana katika nyanja fulani hususan kwenye elimu ya wasichana na haki za kisheria kwa wanawake.Hata hivyo anasema kuna viashirio vingi vibaya ambavyo vinahitaji kushughulikiwa kwa haraka.

Viashirio hivyo ni pamoja na kuendelea kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ukosefu wa fursa za kiuchumi na uwakilishi usiozingatia usawa katika masuala ya kupitisha maamuzi katika nchi zote zile za kimaskini halikadhalika na za kitajiri.

Mjini Beijing viongozi wa serikali walikubaliana kupitisha sera ambazo zitatenga asilimia 30 ya viti vya bunge kwa ajili ya wanawake.Lakini miaka 10 baadae ni asilimia 15 tu ya wabunge duniani ndio wanawake.

Wataalamu wa kiuchumi katika Umoja wa Mataifa na viongozi wa mashirika ya kijamii wamedokeza kwamba wakati mienendo fulani ya kiuchumi duniani imekuwa na taathira nzuri kwa maisha ya wanawake mengine imedhoofisha mapambano yao ya kuwania usawa wa kiuchumi na kisiasa.

Wakati wakitambuwa kwamba kupatikana kwa urahisi teknolojia ya habari kumeongeza fursa za wanawake katika shughuli za mtandao na kiuchumi wanawaona mamilioni ya wakulima wa kike duniani kote wanazidi kuwa maskini zaidi na zaidi hali iliosababishwa na kubadilisha ukulima kutoka ule wa uzalishaji wa mazao ya chakula hadi kuwa wa uzalishaji wa mazao ya biashara.

Baadhi ya wataalamu wanasema mbali ya mienendo hiyo ya utandawazi wa kiuchumi kuendelea kwa mataifa kujiimarisha kijeshi pia kunadhoofisha mapambano ya wanawake kwa ajili ya usawa wa kiuchumi na kisiasa.Hivi sasa mataifa hutumia zaidi ya dola bilioni 900 kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za kijeshi.

Kang na maafisa wengine wa Umoja wa Mataifa inaonekana kuridhika na maendeleo yaliofikiwa kwenye nyanja ya sheria ambayo huwalinda wanawake kutokana na ubaguzi na matumizi ya nguvu(ukatili).Lakini makundi ya kijamii hayakuridhika.

Katika repoti iliyotolewa mwaka jana na kundi la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Equality Now imetaja kwamba licha ya ahadi zilizotolewa mjini Beijing zaidi ya nchi 40 bado zilikuwa haziko tayari kubadili sheria ambazo zinakongomelea ubaguzi dhidi ya wanawake.

Wanawake hukabiliwa na vitendo vya ukatili katika nchi nyingi kwa sababu sheria zinaridhia vitendo kama vile vya mauaji ya heshima,ubakaji kwenye ndoa na wanaume kupiga wake zao.

Siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amezitaka serikali kulipa uzito suala hilo kwa kuongeza maradufu jitihada za kupiga vita ukatili dhidi ya wasichana na wanawake kwa uongozi kuonyesha kwamba linapokuja suala la ukatili dhidi ya wasichana na wanawake hakuna sababu za kuvumiliwa wala visingizio vya kuvumiliwa.

Hivi karibuni Annan pia ametowa repoti kabambe kwa kuzingatia majibu ya nchi 135 juu ya masuali ya kile walichofanya hadi hivi sasa kuendeleza usawa wa kijinsia.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema repoti hiyo itatumika kama kichocheo cha mjadala juu ya utekelezaji wa Sera ya Beijing ya Vitendo.Inalenga katika masuala muhimu kama vile umaskini wa wanawake,elimu,afya,matumizi ya nguvu,mizozo inayohusisha silaha,fursa za kiuchumi,kazi za mikataba na vibaruwa pamoja na kutumika majumbani.

Masuala mengine yaliomo kwenye repoti hiyo ni usafirishaji wa wanawake na wasichana kwa magendo,Virusi vya HIV na UKIMWI na wanawake wa makabila asilia.

Watetezi wa haki za wanawake wanaamini kwamba bila ya kufanikisha usawa wa jinsia malengo hayo hayawezi kufikiwa aidha iwe ni umaskini au ujinga.Mkutano huo utaendelea hadi tarehe 11 mwezi wa Machi wakati wajumbe yumkini wakarudia tena ahadi yao kwa Sera ya Beijing ya Vitendo.