1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : FBI yapekuwa nyumba ya Makamo wa Rais wa Nigeria

28 Agosti 2005
https://p.dw.com/p/CEgr

Makachero wa shirika la upepelezi la Marekani FBI wameipekuwa nyumba ya makamo wa rais wa Nigeria Atiku Abubakar kama sehemu ya uchunguzi wa kimataifa wa kupiga vita rushwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Joanne Moore amesema upekuzi wa nyumba hiyo ilioko katika kiunga cha Maryland cha mji mkuu wa Marekani ulifanyika hapo tarehe tatu Augusti lakini amekataa kutowa ufafanuzi zaidi.

Moore ameliambia shirika la habari la AFP kwamba maulizo yote kuhusu upekuzi wa nyumba hiyo ya makamo wa rais wa Nigeria Atiku Abubakar yanapaswa kufikishwa kwa idara ya sheria.

Maafisa wa idara ya sheria wamekataa kuzungumzia lolote lile juu ya tukio hilo lakini duru zilizozungumza kwa sharti ya kutotajwa jina zimesema upekuzi huo ulikuwa ni sehemu ya uchunguzi wa shirika la upelelezi la Marekani FBI kwa mkataba wa mawasiliano ya simu uliopendekezwa ambao unadaiwa kuihusisha Nigeria pamoja na mbunge wa bunge la Marekani William Jefferson wa Luoisiana.

Kwa mujibu wa repoti makachero wa FBI walikuwa wakitafuta ushahidi wa malipo yasio halali yaliyotolewa au kutayarishwa na mbunge huyo wa chama cha Demokrat kwa ajili ya Abubakar, maafisa wengine wa serikali ya Nigeria pamoja na Makamo wa Rais wa Ghana Alhaji Aliu Mahama.