Watatu washinda tuzo ya Nobel katika nyanja ya Uchumi
11 Oktoba 2010Tuzo ya Nobel katika masuala ya Uchumi kwa mwaka huu imetolewa kwa raia wa Marekani, Peter Diamond na Dale Mortensen pamoja na Muingereza mwenye asili ya Cyprus, Christopher Pissarides kwa kusaidia kuelezea jinsi gani sera za kiuchumi zinavyoweza kuathiri katika suala la ukosefu wa ajira.
Kamati ya uteuzi ya tuzo ya Nobel imewatangaza washindi hao watatu kwa utafiti wao walioufanya katika masoko ambao unasaidia kuelezea jinsi ukosefu wa ajira, upatikanaji wa ajira na mishahara zinavyoathiriwa na sera za kanuni na kiuchumi.
Diamond alichambua msingi wa kile kinachoitwa kutafuta masoko, wakati Mortensen na Pissarides waliongeza wigo wa nadharia hiyo na kuitumia katika soko la ajira. Utafiti huo unajumuisha mifano rahisi ya muuzaji na mnunuzi wa bidhaa pamoja na uhusiano tata kati ya mwajiri na mtafuta ajira au kati ya viwanda na wasambazaji bidhaa.
Diamond mwenye umri wa miaka 70, anafanya kazi katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusettes, huku Mortensen mwenye umri wa miaka 71 akiwa katika Chuo Kikuu cha Kaskazini-Magharibi. Pissarides, mwenye umri wa miaka 61 anajishughulisha katika Chuo cha Uchumi cha London. Washindi hao, Peter Diamond, Dale Mortensen na Christopher Pissarides wametunukiwa Dola milioni 1.5. Tuzo ya Nobel katika masuala ya Uchumi ni tuzo pekee kati ya tuzo sita za Nobel ambazo haijaanzishwa kutokana na wosia wa Alfred Nobel, raia wa Sweden aliyekuwa na viwanda mnamo mwaka 1895.
Tuzo hii ilianzishwa mwaka 1968 kwa ajili ya kuadhimisha sherehe ya mwaka wa 300 wa Benki Kuu ya Sweden na ilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1969. Mwaka uliopita, Elinor Ostrom alikuwa ni mwanamke wa kwanza kushinda tuzo hiyo. Tuzo kubwa kabisa ya Nobel ambayo ni ile ya Amani, ilitolewa Ijumaa iliyopita, akitunukiwa mwanaharakati wa haki za binaadamu raia wa China, Liu Xiabo, huku ikiandamana na wito kutoka pembe mbalimbali za dunia kutaka aachiwe huru. Kwa wakati huu anatumikia kifungo cha miaka 11 jela kwa kuukosoa utawala wa China.
Alhamisi iliyopita, raia wa Peru, Mario Vargas Llosa alishinda tuzo ya Nobel katika masuala ya Fasihi. Msimu wa kutangaza tuzo hizo ulianza Jumatatu iliyopita kwa kutolewa tuzo ya Madawa iliyomwendea Daktari wa Uingereza, Robert Edwards. Tuzo hiyo kwa upande wa Fizikia ilifuatia siku ya Jumanne ambapo waliofanikiwa kujitwalia ni watafiti wazaliwa wa Urusi, Andre Geim na Konstantin Novoselov. Richard Heck wa Marekani na Ei-ichi Negishi na Akira Suzuki wa Japan walishinda tuzo ya Kemia iliyotolewa siku ya Jumatano.
Tuzo ya Amani ya Nobel inatarajiwa kutolewa mjini Oslo, Norway Desemba 10 mwaka huu, ambayo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwanzilishi wa tuzo hiyo Alfred Nobel kilichotokea tarehe kama hiyo lakini mwaka 1896. Washindi wengine wa tuzo za Nobel katika nyanja mbalimbali, watakabidhiwa pia tuzo zao mjini Stockholm, Sweden siku hiyo hiyo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/APE/RTRE)
Mhariri:M.Abdul-Rahman