Watu 167 waangamia katika ajali ya ndege Korea Kusini
29 Desemba 2024Ndege ya abiria ya shirika la Jeju Air iliyowabeba abiria 181 kutoka Thailand kuelekea Korea Kusini, imeanguka usiku wa kuamkia leo ilipokuwa ikitua na kuwaka moto. Watu 167 wamethibitishwa kufariki kwenye ajali hiyo.
Waokoaji wanahofia huenda watu wote waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wameangamia isipokuwa watu wawili ambao wamenusurika.
Chanzo kamili cha ajali hiyo hakijabainika lakini maafisa wametaja hali mbaya ya hewa na ndege kuingia kwenye injini kuwa huenda zikawa sababu.
Video ilisoyambazwa mitandaoni ilionyesha ndege hiyo ikitua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Muan Korea Kusini, kisha ikapoteza mwelekeo huku injini zake zikifuka moshi kabla ya kugonga ukuta, kulipuka na kuwaka moto.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na maafisa wa kupambana na moto kwa familia za watu waliokuwemo ndani ya ndege, nafasi ya abiria waliokuwemo ndani kunusurika ni ndogo.