1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO bado inasubiri data za UVIKO-19 kutoka kwa China

31 Desemba 2024

Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO bado linasubiri ushirikiano kamili kutoka kwa serikali ya China ili kufafanua chanzo cha janga la UVIKO-19. WHO imeitaka China kutoa data zote ili waelewe chimbuko la janga hilo.

https://p.dw.com/p/4ohNd
Askari wa China nje ya maabara ya kuchunguza virusi vya corona mjini Wuhan
Timu ya WHO ilizuru Wuhan mwaka wa 2021, lakini baadhi ya wajumbe walilalamika kwa kutopewa taarifa za kinaPicha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Hii ni miaka mitano baada ya visa vya kwanza vya ugonjwa mpya wa mapafu kuripotiwa katika mji wa China wa Wuhan. WHO imesema jijini Geneva kuwa hilo ni sharti la kimaadili na kisanyasi. Imeitaka China kutoa data zote ili wanasayansi waelewe chimbuko la janga hilo.

Taarifa ya WHO imesema kuwa bila uwazi na ushirikiano miongoni mwa nchi tofauti, dunia haiwezi kuzuia na kujiandaa vya kutosha kwa magonjwa ya milipuko na majanga ya siku za usoni. Tangu kuanza kwa janga la UVIKO-19, China ilikuwa na wasiwasi kuwa ingelaumiwa kwa mripuko huo duniani.

Tangu wakati huo, serikali na vyombo vya habari vya serikali vimekuwa vikifanya kampeni kubwa ya maoni inayozingatia uwezekano kwamba virusi vinaweza kutoka nje ya nchi na sio kutoka China. Ripoti ya mwisho ya jopo la pamoja ya watalaamu wa China na WHO ilisema "inawezekana sana" kwamba kirusi cha corona kilitoka kwa spishi ya wanyama wa porini na kisha kuenea kwa wanyama wengine kabla ya kuruka hadi kwa wanadamu.