Yemen: Saleh asema yuko tayari kufungua ukurasa mpya
3 Desemba 2017Kauli hiyo ya Ali Abdallah Saleh kwamba anataka sasa kuzungumza na utawala wa Saudi Arabia ameitoa wakati ambapo uhusiano wake na kundi la waasi linaloungwa mkono na Iran unalegalega. Wakati hayo yakiendelea wapiganaji wanaomuunga mkono kiongozi huyo wa zamani wa Yemen wanaendelea kupambana na wapiganaji wa kundi la waasi wa Houthi kwa siku ya tano katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa.
Televisheni ya Al Arabiya inayomilikiwa na Saudi Arabia imeripoti kuwa takriban watu 80 wameuawa katika mapigano hayo kati ya wapiganaji waaminifu kwa Saleh na waasi wa Houthi. Migogoro kati ya pande hizo mbili zilizokuwa zamani washirika imeongezeka katika miezi ya hivi karibuni, huku wafuasi wa Saleh wakiwalaumu waasi wa Houthi kwa kujaribu kujiongezea madaraka.
Katika hotuba yake kwenye televisheni Saleh ametoa wito kwa ndugu zake katika nchi jirani wa kuacha vitendo vya uchokozi na badala yake amewaomba waondoe vizuizi dhidi ya Yemen na wao wako tayari kuufungua ukurasa mpya.Saleh pia ameahidi kwamba, baada ya mapigano kusitishwa na vizuizi kuondolewa watakuwa tayari kushiriki katika majadiliano ya moja kwa moja kupitia mamlaka halali inayosimamiwa na bunge la Yemen.
Maoni yake yamepokewa kwa furaha na muungano wa majeshi unao ongozwa na Saudi Arabia. Wahusika katika muungano huo wameeleza kuwa wanayaamini na kuyaunga mkono mapendekezo ya viongozi na wahusika wa chama cha Ali Abdalla Saleh cha General People's Congress (GPC). Saleh na wafuasi wake wanataka kurudisha ushirikiano na nchi za Kiarabu.
Saudi Arabia imekuwa inauongoza ushirikiano wa mataifa ya Kiarabu yanayofuata madhehebu ya Sunni na wamekuwa wakipigana na kundi la waasi linalo muunga mkono Saleh na pia waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran tangu mwanzoni mwa mwaka 2015. Nchi za Kiarabu hivi karibuni ziliweka vizuizi vya kijeshi kote nchini Yemen baada ya waasi wa nchi hiyo kurusha kombora lililofika karibu na mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
Yemen ni mojawapo ya nchi zilizo masikini zaidi duniani. Tangu mwaka 2015, inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Saudi Arabia na washirika wake wanapambana na makundi ya waasi yanayoungwa mkono na Iran. Nchi hiyo imekumbwa na janga la kibinadamu, watu zaidi ya 10,000 wameuawa katika mapigano.
Watu wengine karibu milioni 2 wamelazimika kuyahama makazi yao. Pamoja na hayo mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu umewaathiri takriban watu milioni 1. Wakati huo huo nchi hiyo pia inakabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/p.dw.com/p/2oecM
Mhariri: John Juma