1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen: Saudi Arabia na washirika waishambulia Hodeidah

Daniel Gakuba
13 Juni 2018

Vikosi vinanyoungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia vimeanzisha mashambulizi yenye lengo la kuukamata mji wa bandari wa Hodeidah ambao uko chini ya udhibiti wa waasi wa Kihouthi nchini Yemen.

https://p.dw.com/p/2zR3D
Jemen Saudi-Arabische Truppen
Mashambulizi ya kuikomboa Hodeidah yanatarajiwa kuwa makali zaidi tangu vikosi vinavyoongozwa na Saudi Arabia vilipoingilia kati nchini YemenPicha: picture-alliance/dpa

Tangazo la kuanza kwa operesheni hiyo kubwa limetolewa na serikali ya Yemen inayoishi uhamishoni nchini Saudi Arabia, ikisema vikosi vya ardhini vimenza kuukomboa mji wa Hodeidah, vikisaidia na ndege pamoja na meli za kivita. Operesheni hiyo iliyopachikwa jina la ''ushindi wa dhahabu'' imeanzishwa baada ya muda wa mwisho uliotolewa na Umoja wa Falme za Kiarabu, kwa waasi wa Kihouthi kuwa wameuachia mji huo ulio kwenye Bahari ya Sham, kupita usiku wa kuamkia leo.

Bandari ya Hodeidah ni njia muhimu ya kupitishia msaada wa kibinadamu kuelekea katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya juhudi za kidiplomasia baina ya pande zinazohasimiana kujaribu kuepusha mashambulizi katika mji wa Hodeidah, kwa hofu kwamba yangekwamisha msaada wa chakula, dawa na mafuta kwa Wayemen wengi, ambao tayari wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Hodeidah ni njia ya asilimia 90 ya mahitaji ya Yemen

Jemen Hodeidah Unterernährte Kinder
Vita vya miaka 3 vimeiacha Yemen katika mzozo mkubwa wa kibinadamuPicha: Getty Images/AFP/A. Hyder

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na msaada wa kibinadamu Mark Lowcock amesema asilimia 90 ya mahitaji ya chakula, mafuta na dawa nchini Yemen huagizwa kutoka nje, na kwamba asilimia 70 ya bidhaa zote zinazoagizwa hupitia bandari ya Hodeidah, na ametoa wito wa kutotatiza shughuli zake.

''Watu milioni saba wanategemea bandari ya Hodeidah kwa mahitaji yao yote yanayotolewa na mashirika ya msaada.'' Amesema Lowcock na kuongeza kuwa kitu cha kwanza ambacho wadau wote wanatakiwa kufanya ni kuhakikisha kuwa bandari za Hodeidah na Salif zinafanya kazi bila usumbufu, ili shehena ya msaada wa kibidamu, na bidhaa za kibiashara viendelee kupita kwa viwango vya kutosha.'

Wito kama huo wa Umoja wa Mataifa umetolewa pia na shirika la kimataifa la msalaba mwekundu, ambalo limezikumbusha pande zote zinazopigana majukumu yao chini ya sheria ya kimataifa, kulinda usalama wa raia.

Wahouthi wadai kuzishambulia meli za washirika

US Kampfjet F/A-18C Hornet fliegt einen Angriff
Ndege za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi ArabiaPicha: picture-alliance/dpa/MC3 Josh Petrosino

Kamanda wa vikosi vya waasi hao Mohammed  Ali al-Houthi ambaye ametishia kuzishambulia meli za mafuta zinazopita katika bahari ya Sham, amewaonya washirika wa kijeshi wanaoongozwa na Saudi Arabia kutothubutu kuishambulia bandari ya Hodeidah, na kupitia mtandao wa twitter amesema wapiganaji wake wamezishambulia meli za ushirika huo.

Kituo cha televisheni cha Wahouthi cha al-Masirah kimesema makombora mawili yameuzipiga meli za maadui zao. Bado hakuna taarifa zozote kutoka washirika kuthibitisha wala kukanusha madai hayo.

Haya ni mashambulizi ya kwanza ya ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kwenye mji huo wenye ulinzi mkali, lengo likiwa kuwazingira waasi wa Kihouthi katika mji mkuu ili kuwalazimisha kuja kwenye meza ya mazungumzo.

Ushirika wa kijeshi unaozishirikisha nchi nyingi za Kiarabu uliingilia kati nchini Yemen mwaka 2015, ukudhamiria kuirejesha madarakani serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Abd-Rabbu al-Mansour na inayotambuliwa kimataifa, na kuzuia kujipanua kwa ushawishi wa Wahouthi ambao ni wa madhehebu ya Shia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, ape

Mhariri: Iddi Ssessanga