Zaidi ya wafungwa 1,500 watoroka Msumbiji
26 Desemba 2024Zaidi ya wafungwa 1,500 walitoroka kutoka gereza moja jijini Maputo Jumatano, wakitumia fursa ya siku ya tatu ya machafuko yaliyochochewa na uthibitisho wenye utata wa ushindi wa chama tawala cha Frelimo katika uchaguzi wa hivi karibuni.
Mkuu wa Polisi wa Taifa, Bernardino Rafael, alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa jumla ya wafungwa 1,534 walitoroka kutoka gereza lenye ulinzi mkali lililoko takriban kilomita 15 kutoka mji mkuu.
Soma pia: Watu 21 wauawa kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata Msumbiji
Aliongeza kuwa kati ya waliokuwa wakijaribu kutoroka, 33 waliuawa na 15 walijeruhiwa katika makabiliano na walinzi wa gereza. Operesheni ya kuwatafuta wahalifu hao, iliyosaidiwa na jeshi, ilisababisha kukamatwa kwa takriban watu 150.
Takriban wafungwa 30 kati ya waliotoroka walihusishwa na makundi yenye silaha ambayo yamesababisha machafuko na mashambulizi katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado kwa miaka saba iliyopita.