Ziara ya Kansela Merkel Afrika Kaskazini magazetini
3 Machi 2017Ziara ya kansela Angela Merkel kaskazini mwa Afrika, wito wa spika wa bunge la Ulaya Antonio Tajani wa misaada zaidi kwa Afrika na tuhuma za ubaguzi dhidi ya waafrika nchini Ujerumani zilizotajwa na tume ya Umoja wa mataifa iliyofika ziarani Ujerumani hivi karibuni ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
"Kituo cha muda" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Der Tagesspiegel linalosema "kansela amekwenda Afrika kaskazini, kwa lengo la kulisaidia eneo hilo kuwazuwia wahamiaji wasielekee Ulaya." Hakuna mnamo wakati huu tulio nao eneo lolote jengine linalopewa umuhimu mkubwa zaidi kama hilo la kaskazini mwa Afrika. Kansela Merkel amezitembelea Misri na Tunisia. Der Tagesspiegel limekumbusha ziara ya hivi karibuni ya waziri mkuu wa Tunisia ,Yusuf Shahed mjini Berlin pamoja na ile iliyoakhirishwa ghafla ya kansela Merkel nchini Algeria, kwasababu rais Abdel Aziz Bouteflika alikuwa mgonjwa.
Vituo vya kuwapokea wakimbizi Afrika Kaskazini vinakosolewa
Nchi hizo za Afrika kaskazini zimegeuka kuwa kituo muhimu wanakopitia wahamiaji wanaotaka kuja ulaya. Na hasa watu kutoka kusini mwa jangwa la Sahara au maeneo ya mizozo katika pembe ya Afrika, wanaovuka bahari ya kati kuelekea Italia, na wengine wakielekea pia Uhispania. Makundi ya wahalifu wanaosafirisha watu kinyume na sheria yamepiga kambi zaidi nchini Libya na wengine nchini Misri. Der Tagesspiegel linasema kansela Merkel anataka yafikiwe makubaliano ya ushirikiano pamoja na mataifa hayo, mfano wa yale yaliyofikiwa kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki. Nchi hizo za Afrika kaskazini zinatakiwa ziwazuwie wakimbizi wasielekee Ulaya na ikiwezekana wawatimuwe wanapofika mpakani.
Gazeti linazungumzia pia madai ya wawakilishi wa vyama ndugu vya CDU/CSU na pia baadhi ya wana SPD wanaotaka vijengwe vituo vya kuwapokea wahamiaji katika nchi za Afrika kaskazini. Lakini mpango huo unakabiliwa na upinzani wa Tunisia, Moroko na Algeria pia linamaliza kuandika gazeti la Der Tagesspiegel.
Marshall-Plan kwa Afrika anahimiza spika wa bunge la Ulaya
Tajani anahimiza itolewe misaada zaidi kwa Afrika" linaandika gazeti la mjini Berlin,"Berliner Zeitung". Spika huyo wa bunge la Ulaya anazungumzia umuhimu wa kuanzishwa mpango wa dharura wa kulisaidia bara la Afrika, mfano wa ule ulioanzishwa na Marekani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia-Marshall-Plan."Mabilioni yanahitajika , la sivyo mamilioni ya waafrika wataingia Ulaya katika kipindi cha miaka 20 inayokuja" amenukuliwa Antonio Tijani akisema. Mwanasiasa huyo aliyeshika nafasi ya spika wa zamani wa Bunge la Ulaya Martin Schulz, anashauri ibuniwe mikakati ya kuinua shughuli za kiuchumi na kidiplomasia na kuwapatia matumaini mema wakaazi wa bara la Afrika. Gazeti la Berliner Zeitung limekumbusha mpango kama huo umeshauriwa pia na waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Gerd Müller.
Tuhuma za kubaguliwa waafrika Ujerumani
Lilikuwa gazeti hilo hilo la mjini Berlin,"Berliner Zeitung lililozungumzia lawama za tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wanaofanyiwa waafrika nchini Ujerumani. Tume maalum ya Umoja wa Mataifa inayochunguza tuhuma za ubaguzi dhidi ya jamii za wahamiaji na wakimbizi ulimwenguni, ilikuwa ziarani nchini Ujerumani. Baada ya uchunguzi wameandika ripoti inayozungumzia jinsi watu wenye asili ya Afrika wanavyobaguliwa nchini Ujerumani. Wajumbe wa tume hiyo wameitemelea kwa muda wa wiki moja,miji kadhaa ikiwa ni pamoja na Berlin, Dresden, Frankfurt am Main, Cologne na Hamburg na kuzungumza na wawakilishi wa serikali kuu, serikali za majimbo, wabunge, wawakilishi wa mashirika ya haki za binaadam, mawakili na pia wahusika.
Na wahusika wanalalamika wanasema wanabaguliwa shuleni, wanapotafuta kazi au nyumba na pia wanasema wanabaguliwa na taasisi za serikali mfano wa polisi na kadhalika. Tume hiyo ya wataalam inayoongozwa na Ricardo Sunga wa Philippines ingawa imesifu juhudi za serikali kuu ya Ujerumani za kuupatia ufumbuzi mzozo huo wa ubaguzi, hata hivyo inawahimiza maafisa wa serikali zote, tangu serikali kuu mpaka za majimbo waazinshe mkakati wa kuimarisha hali ya haki za binaadam linamaliza kuandika gazeti hilo la mjini Berlin.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSEM/ALL/Presse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman