Biden atoa hotuba ya kuaga
16 Januari 2025Akitoa hotuba hiyo, Rais Biden aliwaonya Wamarekani na kusema hakuna rais anayepaswa kuwa na kinga ya uhalifu uliofanywa akiwa madarakani na kwamba wanahitaji kurekebisha katiba ili kufanikisha hilo.
Majaji walipitisha uamuzi wa kinga kwa marais wa zamani
Mnamo mwezi Julai, majaji wa Mahakama ya Juu ya Marekani walifanya uamuzi ulioungwa mkono na majaji sita na kupingwa na watatu ya kuwapa kinga kubwa marais wa zamani dhidi ya kushtakiwa kwa makosa ya jinai kwa vitendo rasmi, hatua iliyoashiria ushindi mkubwa kwa Trump.
Biden aonya kuhusu ushawishi usiodhibitiwa
Biden pia amesema kuwa watu wenye ushawishi wanataka kutumia ushawishi wao usiodhibitiwa, kupinga hatua ambazo zimechukuliwa kukabiliana na mzozo wa mabadaliko ya tabianchi ili kukidhi maslahi yao ya kibinafsi kwa ajili ya ushawishi na faida.
Biden awataka Wamarekani "kutuliza joto la kisiasa"
Rais huyo ameongeza kuwa hawapaswi kushurutishwa katika kukatisha tamaa ya mustakabali wa maisha yao, watoto wao na wajukuu wao.
Kuhusu suala la akili mnemba,Bidenamesema katika enzi ya sasa ya matumizi ya akili hiyo mnemba, ni muhimu zaidi kuliko awali kwamba kama taifa huru, Marekani na sio China, lazima iongoze ulimwengu katika maendeleo ya sekta hiyo.
Akizungumzi suala la kodi, Biden amesema lazima wafanyie marekebisho kanuni za kodi sio kwa kutoa punguzo kubwa la kodi kwa mabilionea, lakini kwa kuwafanya waanze kulipa mgao wao wa haki. Raishuyo pia ameongeza kuwa wanahitaji kupata pesa zilizopatikana kwa njia zisizohalali zinazotumika kufadhili michango mingi ya kampeni na kuziondoa kwenye siasa za nchi hiyo.
Biden atetea rekodi ya sera yake ya kigeni licha ya mizozo inayoendelea
Biden pia ameelezea kuwa wanaendelea kuiimarisha jumuiya ya kujihami ya NATO, Ukraine bado iko huru, na walipiga hatua mbele katika ushindani kati ya Marekani na China.
Biden awashukuru raia wa Marekani
Rais huyo alimalizia hotuba yake kwa kuwashukuru raia wa Marekani huku akisema kwamba baada ya miaka 50 ya utumishi wa umma, aliwapa ahadi na kwamba bado anaamini misingi ya taifa hilo ambapo nguvu ya taasisi zake na mienendo ya watu wake ni muhimu.
Bidenaliwataka raia wa nchi hiyo kuwa imara na kudumisha imani yao kwa taifa hilo. Wakati huo huo, aliwatakia kila la heri na kusema anaipenda Marekani huku akimuomba Mola awabariki wote.