Chama cha CDU kumchagua mrithi wa Merkel Januari
1 Novemba 2020Baada ya mazungumzo ya kina, wagombea watatu wa nafasi hiyo wameitaka bodi ya utendaji ya chama hicho kufanya mkutano huo Januari. Wagombea hao ni mfanyabiashara wa zamani na kiongozi wa CDU bungeni Friedrich Merz, Waziri mkuu wa jimbo la North-Rhine Westphalia Armin Laschet na mtaalam wa masuala ya mambo ya nje katika chama hicho Norbert Roettgen.
Mkutano huo wa wanachama 1001 ulikuwa umepangiwa kufanyika mwezi Disemba 4 ila uliahirishwa Jumatatu kwa sababu idadi ya maambukizi ya virusi vya corona inaongezeka Ujerumani na majimbo ya nchi hiyo yameweka vikwazo vipya.
Kuahirishwa kwa mkutano huo kulizua mgawanyiko baina ya wagombea hao watatu huku Friedrich Merz akiwatuhumu baadhi ya watu katika uongozi wa chama hicho kumpinga asiuchukue wadhfa huo.
Wagombea wanapendelea mkutano ufanyike uso kwa uso
Lakini Katibu Mkuu Ziemiak ametoa wito wa umoja katika chama.
"Umoja katika CDU ni muhimu kwa Ujerumani hasa katika nyakati ngumu kama hizi," alisema Ziemiak.
Katibu huyo mkuu ameongeza kuwa wagombea hao wanapendelea mkutano wa uso kwa uso ila kama hilo halitowezekana basi ufanyike kwa njia ya video huku kura zikipigwa kidijitali.
Ziemiak amesema hatua za mwisho za jinsi mkutano huo utakavyofanyika zitaamuliwa Disemba 14.
Angela Merkel mwenye umri wa miaka 66 amesema hatogombea tena Ukansela katika kipindi kijacho cha mapukutiko baada ya kuwa uongozini tangu mwaka 2005 na kuthibitishwa kupendwa na wapiga kura wa Ujerumani.
Kura za maoni zinaonyesha Merz ana umaarufu mkubwa miongoni mwa wanachama wa CDU kuliko Laschet na Roettgen ila wakuu wa chama hicho ambao wana uhusiano wa karibu na wawakilishi wanampendelea Laschet.
CDU ndicho chama kikubwa zaidi katika bunge la Ujerumani, Bundestag
Chama hicho kimekuwa katika mzozo wa kiuongozi tangu mwenyekiti wa sasa Annegret Kramp-Karrenbauer ambaye alimrithi Merkel katika uongozi wa chama hicho mwaka 2018 kusema mwezi Februari kuwa hatogombea ukansela mwakani na kwamba ataiacha hiyo nafasi ya mwenyekiti.
Chama cha CDU ndicho chama kikubwa zaidi katika bunge la Ujerumani, Bundestag, na kuwa kiongozi wa chama hicho inaonekana kuwa kama mwanzo wa kuchukua mikoba ya Kansela Angela Merkel kama kiongozi wa serikali ya nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Ulaya.
Ujerumani ni sharti ifanye uchaguzi wa shirikisho kufikia Oktoba 24 mwaka 2021.