1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Ethiopia na Somalia kufanya mazungumzo ya kumaliza mzozo

12 Desemba 2024

Ethiopia na Somalia zimekubaliana kufanya mazungumzo "yaliotajwa kuwa ya kiufundi" ili kuutatua mzozo uliochochewa kufuatia makubaliano ya bandari kati ya Ethiopia na eneo lenye utawala wa ndani la Somaliland.

https://p.dw.com/p/4o3lW
Turkish President Erdogan, Somali President Mohamud and Ethiopian Prime Minister Ahmed hold a joint press conference
Rais wa Uturuki Reccip Tayyip Erdogan (katikati) akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kulia) na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud katika mkutano na waandishi habari mnamo Disemba 11, 2024 mjini Ankara baada ya mazungumzo ya kuutanzua mzozo kati ya Somalia na Ethiopia. Picha: Murat Kula//TUR Presidency/Handout/Anadolu/picture alliance

Uturuki imeongoza juhudi za upatanishi kati ya Ethiopia na Somalia katika wakati ambapo mvutano umekuwa ukiongezeka kati ya nchi hizo mbili baada ya Addis Ababa kusaini makubaliano ya maelewano na Somaliland mwezi Januari.

Makubaliano hayo yaliyotajwa kuwa ya kihistoria yanairuhusu Ethiopia kutumia bandari kuu katika eneo la Somaliland kwa mabadilishano ya Ethiopia kuitambua Somaliland kama nchi huru, hatua ambayo Somalia imeeleza kuwa ni ukiukwaji wa uhuru na mipaka yake.

Makubaliano ya kuutatua mzozo huo yalifikiwa baada ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kufanya mikutano tofauti na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed jana Jumatano.

Katika makubaliano hayo, pande zote mbili - Ethiopia na Somalia - zimekubaliana kufanya mazungumzo yatakayoanza mnamo Februari mwaka 2025 na kukamilika ndani ya miezi minne, na yataheshimu pia mipaka ya Somalia.

Pia miongoni mwa masuala walioafikiana ni kwamba, nchi hizo mbili zitafanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia "makubaliano ya kibiashara yenye manufaa kwa pande zote mbili" na kuiruhusu Ethiopia kuifikia bahari chini ya mamlaka ya Somalia.

Erdogan asifu utayari wa pande hizo mbili kutafuta suluhu ya mzozo

Erdogan, akiandamana na viongozi wa Somalia na Ethiopia ubavuni mwake, amewaambia waandishi wa habari mjini Ankara kwamba pande hizo zimefika "hatua muhimu" katika juhudi za kuutatua mzozo kati yao.

Rais huyo wa Uturuki ameeleza kwamba yaliyopita yamepita na sasa ni wakati wa kuganga yajayo.

"Kwa kuzingatia michango na hoja muhimu zilizotolewa na nchi zote mbili, tumekubaliana kwa maandishi na kuandaa tamko la pamoja. Makubaliano hayo yanazingatia kanuni ambazo nchi hizi mbili rafiki, na ambazo ni muhimu sana kwetu, kwa kuangalia mbele na sio kujikita kwa yaliyopita, ili tujenge mustakabali mzuri.” amesema Erdogan.

Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini haijatambuliwa kimataifa wala na Umoja wa Afrika kama taifa huru. Somalia bado inaichukulia Somaliland kama sehemu ya himaya yake.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amesema eneo la Pembe ya Afrika ni tete na ambalo linahitaji Ethiopia na Somalia kufanya kazi kwa ushirikiano kwa manufaa ya pande zote.

Uturuki imejenga uhusiano wa karibu na Somalia na hivi karibuni ilitia saini makubaliano ya kushirikiana katika sekta za ulinzi na tafiti katika uchimbaji wa gesi na mafuta.

Uturuki pia ina uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na Ethiopia.