1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madai ya ugaidi katika jeshi la Ujerumani

9 Mei 2017

Maafisa nchini Ujerumani wamemkamata mwanajeshi wa pili akidaiwa kuwa sehemu ya wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia waliopanga njama ya kufanya shambulizi dhidi ya wanasiasa mashuhuri nchini humo.

https://p.dw.com/p/2chKg
Deutschland Presseerklärung Bundesanwaltschaft | Frauke Köhler
Msemaji wa mwendesha mashtaka wa serikali ya Ujerumani, Frauke KoehlerPicha: picture alliance/dpa/U. Deck

Wanajeshi hao walikuwa wanadaiwa kutaka kufanya mashambulizi hayo kisha wawasingizie wakimbizi kwa shambulizi hilo. Msemaji wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali kuu ya Ujerumani, Frauke Koehler, alisema Maximilian T mwenye umri wa miaka 27, alikamatwa katika mji wa kusini magharibi wa Kehl Jumanne, kwa madai ya kuandaa kitendo cha vurugu.

Gazeti la Ujerumani la Der Spiegel lilisema T ambaye jina lake la mwisho halikutajwa kufuatana na sheria za faragha, ni mwanajeshi aliyekuwa katika kikosi cha wanajeshi walioko katika kambi ya Illkirch, karibu na mpaka wa Kehl na alikuwa katika kambi moja na Franco A, mwanajeshi wa kwanza wa Ujerumani aliyekamatwa, kwa kujifanya kama mkimbizi kwa nia ya kufanya shambulizi la kigaidi.

Maswali yameibuka kuhusiana na propaganda za kinazi katika jeshi la Ujerumani

"Mtuhumiwa anashukiwa kupanga shambulizi pamoja na Franco A na Mathias F waliokamatwa tayari mwezi Aprili," alisema Frauke Koehler, "shambulizi lililochochewa na mtazamo wa mrengo wa kulia."

Verteidigungsministerin Ursula von der Leyen
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen akizungumza na wanajeshi wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/M. Schutt

Suala hilo limezusha maswali kuhusiana na kiasi gani propaganda za mrengo wa kulia zimeenea katika jeshi la Ujerumani - Bundeswehr, na ni kwanini vitengo husika Ujerumani havikuweza kugundua kwamba Franco A alikuwa anajifanya kuwa mkimbizi kutoka Syria.

Katika taarifa, waendesha mashtaka walisema Franco A alipanga kufanya shambulizi hilo mwenyewe na kwa kujifanya mkimbizi kutoka Syria, yeye na wenzake walikuwa wanataka lawama iwaendee watafuta hifadhi waliojiandikisha nchini Ujerumani. Kwa sasa mwanajeshi huyo anazuiliwa akisubiri kufunguliwa mashtaka.

Kambi za wanajeshi zimefanyiwa uchunguzi kutafuta kumbukumbu za kinazi

Frauke Koehler vile vile amesema washukiwa walikuwa wameorodhesha malengo yao ya kufanya mashambulizi.

"Washukiwa walikuwa wameorodhesha malengo yao ya kushambulia katika vitengo A, B, C, na D," alisema Koehler. "Kitengo A kilikuwa kinamlenga aliyekuwa rais wa Ujerumani, Joachim Gauck na waziri wa sheria Heiko Maas."

Russland Ankunft Angela Merkel in Sotschi
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Tukio hilo limelipuka na kuwa sakata kubwa kuhusiana na itikadi kali za mrengo wa kulia katika jeshi la Ujerumani, suala lililopelekea kambi zote za wanajeshi nchini Ujerumani kufanyiwa uchunguzi kutafuta kumbukumbu za kinazi.

Kesi hiyo pia imeiwekea shinikizo serikali ya Kansela Angela Merkel miezi mitano kabla uchaguzi, huku swahiba wake wa karibu waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen, akishutumiwa kwa kushindwa kuliongoza vyema jeshi la Ujerumani.

Mwandishi: Jacob Safari/DPA/Reuters/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga