1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Mwaka 2020 ndio mgumu zaidi wa uongozi wangu

31 Desemba 2020

Kansela Angela Merkel katika hotuba yake mwaka mpya kwa Ujerumani, amewashambulia wale wanaopinga uwepo wa virusi vya corona, amesisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa jamii tofauti na pia ametoa ujumbe wa matumaini.

https://p.dw.com/p/3nOga
Deutschland Neujahransprache der Kanzlerin | Angela Merkel
Picha: Markus Schreiber/REUTERS

Kansela huyo wa Ujerumani amesema bayana kwamba mwaka mzima wa 2020 ndio umekuwa mwaka wenye changamoto chungunzima katika uongozi wake wa miaka 15.

"Sidhani kama natia chumvi ninaposema: hakuna mwaka ambao umekuwa mgumu katika miaka yangu 15 ya uongozi kama mwaka huu unaoelekea kuisha," alisema Merkel katika hotuba hiyo ya kila mwaka inayosikilizwa na kutazamwa na mamilioni ya watu.

Katika janga ambalo limeukumba ulimwengu mzima, Wajerumani milioni 1.7 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 32,000 kufariki dunia. Na idadi inaongezeka kwani mnamo Jumatano zaidi ya watu elfu moja walifariki katika kipindi cha saa ishirini na nne hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa janga lenyewe.

"Janga la virusi vya corona ndio changamoto kubwa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya karne hii," amekiri Merkel. "Ni mzozo wa kihistoria ambao umehitaji mengi kutoka kwetu sote na mengi zaidi kwa baadhi ya watu, najua suala hili linahitaji uaminifu na subra kubwa kutoka kwenu, kutahitajika mwonyesho wa nguvu zaidi na kwa hilo ninawashukuru kwa moyo wangu wote."

Amewashambulia wanaopinga uwepo wa virusi vya corona

Kansela Merkel ameitaja kazi ambayo imefanywa na wahudumu wa afya katika kupambana na janga hili ila pia akawataja wafanyakazi wengine waliokuwa muhimu mwaka 2020.

Deutschland Covid-19 | PK im Bundeskanzleramt Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

"Watu wengi wametusaidia tuendelee na maisha yetu katika janga hili," alisema Merkel. "Katika maduka ya jumla na watu wanaofanya kazi za kusafirisha bidhaa, wafanyakazi wa posta, mabasi na treni, maafisa wa polisi, shule na chekechea, makaisa na waandishi wa habari," aliongeza Kansela huyo.

Merkel amewashambulia pia wale wanaopinga kuwepo kwa virusi vya corona akisema vuguvugu la watu hao limekuwa maarufu miongoni mwa watu wachache nchini Ujerumani huku maelfu ya watu wakifanya maandamano ya kupinga uvaaji wa lazima wa barakoa na vikwazo vyengine katika maisha ya kawaida. Amesema baadhi wanaamini kwamba chanjo ya corona ni kwa ajili ya kudhibiti idadi ya watu au kwamba hakuna kabisa virusi vya corona.

"Nadharia za uovu na njama sio tu ni uongo bali ni hatari na pia ni ujinga na ukatili kwa watu wanaoomboleza," alisema Merkel.

Kansela huyo pia amerudia ahadi yake kwamba atapokea chanjo wakati wake utakapofika. Kinyume na nchi kama Marekani, Ujerumani haikuwaorodhesha wanasiasa wa ngazi ya juu miongoni mwa watu watakaopokea chanjo hiyo wa kwanza.

Chanjo ya BioNTech-Pfizer ambayo ilikuwa ya kwanza kuidhinishwa na kutolewa duniani, ilitengenezwa katika mji wa Ujerumani wa Mainz na Merkel binafsi amewapongeza wanasayansi ambao ni wapenzi na wenye asili ya Uturuki waliohusika katika kuibuni chanjo hiyo.

"Wavumbuzi (wa BioNTech) Ugur Sahin na Ozlem Tureci mjini Mainz waliniambia kwamba kuna watu kutoka nchi sitini duniani wanaofanya kazi katika kampuni yao," alieleza Kansela huyo. "Huo ndio mfano bora wa kwamba ushirikiano wa Ulaya na kimataifa na nguvu ya ushirikiano wa watu tofauti ndio mambo yanayoleta maendeleo."

Ugur Sahin und seine Frau Özlem Türeci
Wavumbuzi wa chanjo ya BioNTech-Pfizer Ugur Sahin na Ozlem TureciPicha: Stefan F. Sämmer/imago images

Mwaka wa mwisho wa Merkel

Licha ya machungu yaliyoletwa na mwaka 2020 Kansela Merkel amejikita katika matumaini ambayo anaamini yatakuja na mwaka 2021. Hii ndiyo mara ya mwisho pia ambapo Merkel anaukaribisha mwaka mpya kama kiongozi wa Ujerumani.

"Mwisho kabisa wacha niseme kitu binafsi: Uchaguzi wa bunge wa Ujerumani utafanyika katika kipindi cha miezi tisa ijayo na sitosimama tena," alisema Kansela huyo ambaye amekuwa madarakani tangu 2005. "Na ndio maana leo, ndiyo natoa hotuba a mwisho kabisa ya mwaka mpya kama Kansela wa Ujerumani."

Alipokuwa akimalizia hotuba yake, Merkel alisalia kuwa mwenye matumaini.

"Licha ya wasiwasi uliopo na hata kutoaminiana, hakuna wakati ambapo tumekuwa na matumaini yanayokuja na mwaka mpya kama sasa," alisema. "Kwa hiyo kwa moyo wangu wote nawatakia nyote pamoja na familia zenu, afya, imani na baraka za mwenyezi Mungu kwa mwaka 2021."