1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ukraine na Urusi: Mashambulizi na diplomasia

3 Januari 2025

Urusi imefanya mashambulizi makubwa ya droni nchini Ukraine usiku wa kuamkia Ijumaa, ikilenga mikoa tisa ikiwemo Kyiv, Donetsk, na Chernihiv. Jeshi la Ukraine nalo limesema limeshambulia kituo cha kamandi ya Urusi Kursk.

https://p.dw.com/p/4omx2
Ukraine | Matokeo ya shambulizi ya Urusi Kyiv
Mashambulizi ya Urusi yamesababisha uharibifu mkubwa wa majengo ya makaazi mjini Kyiv.Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Katika mkoa wa Kyiv, vipande vya mabaki ya droni vilimuua dereva wa lori na kuwajeruhi watu wanne, wakiwemo kijana wa miaka 16. Nyumba za makazi na majengo ya biashara ziliharibiwa katika mikoa kadhaa, ingawa hakuna majeruhi walioripotiwa Kyiv.

Jeshi la Ukraine limeripoti kushambulia kituo cha kamandi ya jeshi la Urusi huko Maryino, mkoa wa Kursk, siku ya Alhamisi, ambako vikosi vya Ukraine vinadhibiti maeneo makubwa baada ya uvamizi wa mwaka uliyopita.

Video zilizotolewa na Ukraine zilionyesha uharibifu wa vituo vya Urusi, huku maafisa wa Urusi wakiripoti mashambulizi ya makombora yaliyosababisha uharibifu wa majengo ya makazi na ya umma. 

Jeshi la Urusi kwa upande wake pia limedai kudungua makombora na droni nyingi za Ukraine zilizolenga mikoa ya mpakani.

Mkoa wa Urusi wa Kursk | Uharibifu
Mashambulizi ya Ukraine yameuathiri pakubwa mkoa wa Kursk wa Urusi.Picha: Yevgeny Martynov/Tass/IMAGO

Zelenskiy asema Trump anaweza kumaliza vita

Rais Volodymyr Zelensky ameonyesha matumaini ya tahadhari kuhusu hali ya kutotabirika ya Rais mteule wa Marekani Donald Trump, akisema inaweza kusaidia kumaliza vita na Urusi.

Soma pia: Russia yafanya mashambulizi ya "kinyama" ya Krismas, Ukraine yasema

"Trump anaweza kuwa mwenye maamuzi thabiti. Kwetu sisi, hili ndilo jambo muhimu zaidi. Sifa zake zipo kweli. Ana uwezo wa kumzuia Putin au, kwa usahihi zaidi, kutusaidia kumzuia Putin. Anaweza kufanya hili," alisema Zelenskiy katika ujumbe wake wa usiku wa vidio.

Zelensky pia ameiunga mkono wazo la Ufaransa na mataifa mengine kupeleka walinda amani nchini Ukraine kuhakikisha amani ya baadae na Urusi ikiwa itatokea, lakini amesisitiza hili litahitaji kuwa hatua kuelekea kujiunga na jumuiya ya NATO. 

Pendekezo la Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu kupeleka majeshi ya Magharibi nchini Ukraine linaendelea kujadiliwa, huku Zelensky akisisitiza ushirikiano mpana wa NATO.

EU: Usambazaji wa gesi ni tulivu licha ya uamuzi wa Ukraine

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umeripoti kuwa usambazaji wa gesi ni salama licha ya Ukraine kusitisha usafirishaji wa gesi ya Urusi kupitia ardhi yake.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

Pamoja na hakikisho hilo kutoka Umoja wa Ulaya, changamoto bado zinayakumba mataifa kama Moldova isiyo mwanachama wa Umoja huo na Slovakia iliyo mwanachama, ambayo imeapa kuichukuliwa hatua Ukraine kujibu uamuzi wake.

Soma pia: Putin asema Urusi itatimiza malengo yote yaliyowekwa Ukraine

Poland, ambayo inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, imesisitiza matumizi ya njia mbadala na mifumo ya kuhifadhi kuhakikisha usambazaji wa gesi unadumu.

Mgogoro kati ya Urusi na Ukraine unaendelea kupamba moto, ukihusisha mashambulizi makali ya droni, mashambulizi ya kujibu ya kimkakati, na juhudi za kidiplomasia.

Huku Ukraine ikikabiliwa na uchovu wa kijeshi na mipango mipya ya kimkakati, msaada wa kimataifa utakuwa muhimu katika kuamua mwelekeo wa vita hivi.