1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande zinazo zozana Yemen zaalikwa kwa mazungumzo

3 Agosti 2018

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen amesema atazialika pande mbili zinazo zozana kwa mazungumzo mjini Geneva, Septemba 6 katika harakati za kuanza mpango wa amani.

https://p.dw.com/p/32Zes
Yemen - al-Hudaida - Soldat
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Gambrell

Yemen ambayo ni mojawapo ya nchi za Kiarabu zenye umaskini wa kupindukia imejikuta katika mapambano ya kuwania madaraka kati ya serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran kwa zaidi ya miaka minne sasa.

"Baada ya kujadiliana na pande husika, kwa sasa napanga kuwaalika Geneva Septemba 6 kwa raundi ya kwanza ya mazungumzo," alisema Griffiths. "Mazungumzo haya yatatoa nafasi kwa pande hizo kujadili mpango wa majadiliano, kukubaliana kuhusu hatua za kuleta imani na mipango maalum ya kuusogeza mpango huu mbele," aliongeza mkuu huyo.

Hakuna mpango wa siku zijazo wa kuwalinda raia

Hiyo ni kauli ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Martin Griffiths alipokuwa akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mwezi uliopita Griffiths alikutana na Rais wa Yemen Abdu Rabu Mansour Hadi kisha baadaye akakutana na kiongozi wa waasi Abdel Malek al-Houthi. Umoja wa Mataifa bado unajaribu kuzuia mapambano kamili kwa ajili ya bandari ya Hodeida, ambayo duru za kijeshi zinasema imekuwa kitovu cha vita hivyo.

Shambulizi la hewani Hodeidah
Mhanga wa shambulizi la hewani lililofanywa YemenPicha: Reuters/A. Zeyad

Mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa John Ging ameonya kwamba hakuna mpango wa siku zijazo wa kuwalinda raia iwapo machafuko katika jimbo la Hodeida yatazidi.

Hayo yakiarifiwa maafisa wa matibabu wa Yemen wamesema muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia unaopambana na waasisi wa Kishia wa Yemen wamefanya mashambulizi ya angani katika bandari ya Hodeida na kuwauwa karibu watu 28 na kuwajeruhi wengine 70.

Kulingana na maafisa hao mashambulizi hayo ya hewani yamefanyika karibu na hospitali ya umma ya mji huo al-Thawra na karibu pia na soko maarufu la samaki. Huyu hapa ni mmoja wa walioshuhudia na kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.

"Nilikuwa naokoa watu ndipo shambulizi la pili la ndege lilipofanywa. Vigae viliangukia usoni na kunifanya nitoke damu kidogo, mkono wangu ulikufa ganzi kutokana na kuangukiwa na vigae hivyo," alisema mhanga huyo.

Mapigano dhidi ya Wahouthi yamekuwa yakiendelea kwa miaka mitatu sasa

Msemaji wa muungano huo wa kijeshi Kanali Turki al-Malki amekiambia kituo kinachomilikiwa na Saudi Arabia cha Al Arabiya kwamba hawakufanya mashambulizi yoyote Hodeida na akaelekeza lawama kwa waasi wa Kihouthi. Alisema muungano huo unafuata utaratibu wa mapambano ulio wazi na wenye msingi wa sheria za kimataifa.

Shambulizi la hewani Hodeidah
Uharibifu uliofanywa na mashambulizi ya hewani huko YemenPicha: Reuters/A. Zeyad

Saudi Arabia, nchi za Umoja wa Kiarabu na marafiki zake wa Kisunni wamekuwa wakipigana nchini Yemen kwa zaidi ya miaka mitatu sasa dhidi ya Wahouthi, huku wakiungwa mkono na mataifa ya Magharibi. Wahouthi wanamiliki sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen ikiwemo Mji Mkuu Sanaa na waliipeleka uhamishoni serikali yao iliyokuwa inaungwa mkono na serikali mwaka 2014.

Kundi la Wahouthi walioko Yemen wanasema wamesema wanasitisha machafuko katika Bahari ya shamu kwa wiki mbili ili kuunga mkono juhudi za amani, siku chache baada ya Saudi Arabia kusitisha kuuzwa kwa mafuta katika nchi za nje kupitia Bahari ya Shamu kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na Wahouthi katika meli za kusafirishia mafuta Julai 25.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/APE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef